Amnesty International yaanika maovu ya askari wa Burundi
24 Agosti 2015Visa hivyo vilikuwa ni moja wapo ya vitendo vya kukandamiza upinzani wakati wa harakati za Rais Pierre Nkurunziza kutafuta kuchaguliwa tena kwa muhula wa tatu.
Ushahidi uliorekodiwa na shirika hilo katika taarifa yake unaonekana kulishutumu jeshi la polisi na idara ya usalama wa taifa nchini humo ( SNR ) kwa kuwatesa na kufanya vitendo vingine vibaya vya kikatili tangu mwezi Aprili mwaka huu dhidi ya makundi ya watu waliokuwa wakishukiwa kupinga uamuzi wa Rais Nkurunzinza wa kuwania muhura wa tatu wa uongozi.
Askari polisi nchini humo walitumia nyaya za umeme wakati maafisa wa idara ya usalama wa taifa walitumia vyuma ikiwa ni pamoja na kuwalazimisha watu waliowakamata kupita katika maji machafu, imesema taarifa hiyo iliyopewa kichwa cha habari, "Hebu Niambie Nitubu Nini!".
Shahidi mmoja abakizwa uchi wa mnyama
Mmoja wa watu waliokamatwa katika kipindi hicho katika taifa hilo la Afrika ya kati mwezi June aliwaonesha maafisa wa shirika hilo la Amnesty alama zilizotokana na suruba alizopata kipindi hicho ambazo zilianza kwa kupigwa na chuma kabla ya kuvuliwa nguo na hatimaye kubakishwa uchi kama alivyo zaliwa.
" Walichukua chombo cha lita tano kilichojazwa mchanga na kukifunga katika sehemu zangu za siri kwa muda wa takribani saa moja na hatimaye nilizirai. Alisema mwanaume mmoja katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa jijini Nairobi nchini Kenya.
Baadae walinikarisha katika maji yaliyotohama yaliyotiwa tindikali ama kwa hakika niliungua sana . Alisema mtu huyo.
Mwandishi mmoja wa habari nchini Burundi Esdras Ndikumana (54) ambaye ni mwakilishi wa shirika la habari la Ufaransa na Radio France International (RFI) ni miongoni mwa watu waliopigwa na maafisa wa idara ya usalama wa taifa kwa karibu saa mbili. Ushahidi wake pia umehusishwa katika taarifa hiyo.
Watuhumiwa wanyimwa haki za msingi
Watu hao waliokamatwa na kuwekwa kizuizini walikumbana na vitendo vya aina mbalimbali vya ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kukamatwa pasipo kufuata sheria, kuwekwa kizuizini, kuteswa na kufanyiwa vitendo vingine vibaya ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kukutana na wanasheria wao, madakitari na pia ndugu zao wa familia, taarifa hiyo iliongeza.
Hatua ya Rais Nkurunzinza ya kuongeza muhula watatu wa uongozi imelalamikiwa na vyama vya upinzani nchini humo ya kuwa imekwenda kinyume na katiba ya nchi hiyo na kusababishwa kupingwa kwa kiwango kikubwa na makundi mbalimbali nchini humo.
Kumekuwepo na matukio ya mauaji kadhaa tangu kuchaguliwa kwake kwa mara nyingine tena likiwemo tukio la kuvamiwa na kuawa kwa mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama mwezi uliopita.
Nkurunzinza ambaye ni muasi wa zamani katika harakati za mapambano ya kisiasa nchini humo na mkiristo aliyezaliwa upya na anae amini kuwa yuko madarakani kwa uwezo wa mwenyezi Mungu aliapishwa juma lililopita kuwa Rais wa nchi hiyo ambapo baada ya kuapishwa kwake aliwaonya wapinzani ya kuwa wata adhibiwa na Mungu. Hakufafanuwa zaidi.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE
Mhariri : Mohammed Abdul-rahman