1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yailaumu polisi kwa watu kupotea

14 Aprili 2016

Wanaharakati wa iBurundi wanafanya kampeni katika mtandao wa intaneti kuuzindua ulimwengu kuhusu kile wanachosema ni kuongezeka kwa matukio ya watu kupotezwa na polisi na maafisa wa usalama wa taifa nchini humo.

https://p.dw.com/p/1IVBs
Burundi Polizei Sicherheitskräfte Militär Symbolbild
Picha: picture-alliance/AA/N. Renovat

Wakati maafisa wa usalama nchini Burundi wanapofika mahala kumtafuta mtu fulani, hawatoi hata waranti wa kumkata. Na wanapomkamata mshukiwa, jamaa wa familia wenye hofu walioachwa nyuma hubaki wakitumai mtu wao atashikiliwa katika gereza linalifahamika. Hii ni kwa sababu mahabusi zisizo rasmi zimekuwa vyumba vya kifo katika miezi tangu rais Pierre Nkurunziza aliposhinda awamu ya tatu.

Katika machafuko hayo, ambapo watu zaidi ya 400 wameuliwa tangu Aprili mwaka uliopita, mtandao wa wanaharakati wa Burundi umeilaumu idara ya polisi ya nchi hiyo kwa kuhusika na visa vya watu kupotea. Wanaharakati hao wanafanya kampeni katika mtandao wa mawasiliano wa intaneti kuuzindua ulimwengu kuhusu kile wanachosema ni kuongezeka kwa matukio ya watu kupotezwa na polisi na maafisa wa usalama wa taifa nchini humo, wakidai kwamba baadhi ya maafisa hao hudai viwango vikubwa vya fedha kutoka kwa familia zinazotaka kuwakomboa jamaa zao.

Kundi la wanaharakati wa Burundi linalojiita, iBurundi, lina wafuasi takriban 11,000 katika mtandao wa kijamii wa Twitter. Wafuasi wake ni wasomi vijana wakiwemo waandishi wa habari, mawakili, wanauchumi, wachambuzi wa sera, na wanafunzi kadhaa. Hayo ni kwa mujibu wa mwanachama mmoja wa kundi hilo aliyekataa kutajwa jina kwa kuhofia usalama wake wakati alipozungumza na shirika la habari la Associated Press, AP.

"Hatujakuwa tukihesabu visa vya watu kupotea lakini wanafikia mamia kadhaa. Wiki mbili zilizopita tunafahamu kuhusu visa 26 vilivyoripotiwa. Baadhi ya watu hawa walipatikana katika magereza yanayofahamika na wengine hawajulikani waliko." alisema mwanachama huyo. Pia alisema kundi la iBurundi linauhimiza Umoja wa Mataifa kuyachunguza magereza yasiyo rasmi kote Burundi ambako inasemekana wafungwa wanateswa na kuuliwa.

Maafisa wadai fidia

Kwa mujibu wa kundi hilo dola kati ya 250 na 2,500 za kimarekani hutakikana kutoka kwa familia zenye matumaini ya kuhakikisha jamaa zao wanaozuiwa wanaachiwa huru. Katika akaunti yake ya Twitter iBurundi imekuwa ikichapisha majina ya watu wanaoaminiwa hawajulikani waliko baada ya kutiwa mbaroni na maafisa wa usalama.

Serikali ya Burundi imekanusha mara kwa mara kwamba inawatesa na kuwaua raia, ingawa Rais Pierre Nkurunziza amevihimiza vikosi vya usalama kutumia kila mbinu zinazohitajika kukomesha machafuko yaliyoanza mwaka mmoja uliopita, wakati raia walipoingia mabarabarani kuandamana wakipinga uamuzi wake wa kugombea awamu ya tatu.

Burundi Polizeigewalt - Polizei schlägt Jungen
Polisi wakimtandika kijana baada ya kuyatawanya maandamano Bujumbura (26.05.2015)Picha: picture-alliance/dpa/D. Kurokawa

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, katika operesheni ya kuwapokonya watu silaha kwenye baadhi ya vitongoji, kama vile Musaga na Nyakabiga, katika mji mkuu Burujumbura, idadi ya watu walioikimbia nchi ilifikia 250,000 mwezi Machi mwaka huu.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yana wasiwasi idadi ya watu wanaopotea na kuuliwa bila hatia huenda inaongezeka huku serikali ikijaribu kuwanyamazisha wapinzani na makundi angalau mawili ya waasi ambayo yamefanya mashambulizi hivi karibuni. "Kimsingi watu wanachukuliwa na maafisa wa polisi au wa ujasusi, na kupelekwa mahali kusikojulikana, halafu hakuna anayesikia taarifa zozote kuwahusu," alisema Carina Tertsakian, mtafiti wa Burundi katika masuala ya haki za binaadamu wa shirika la Human Rights Watch.

Baadhi ya maafisa wa jeshi wanaoonekana kuwa karibu na rais wamelengwa katika mauaji - akiwemo hata mnadhimu mkuu wa jeshi, ambaye aliponea chupu chupu shambulizi la roketi mwaka uliopita - hivyo kuongeza uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Wafungwa wazuiwa katika vituo visivyo rasmi

Baadhi ya wafungwa huenda wanazuiwa katika vituo visivyo rasmi vinavyoendeshwa na wakala wa ujasusi, unaojulikana kama Service National des Renseignements, SNR, na wengine wameuawa na maiti zao hazijaonekana, alisema Carina. Baadhi ya Warundi ambao jamaa wao wamepotea wanasema wanachama wa kundi la waasi linaloiunga mkono serikali linaloitwa Imbonerakure linahusika na baadhi ya visa hivyo.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International liliripoti Januari mwaka huu kwamba kuna makaburi matano ya halaiki katika viunga vya Bujumbura, likinukuu picha za satelaiti, mkanda wa vidio na maelezo ya mashahidi kufuatia mauaji ya Desemba ambayo yanadaiwa yalifanywa na vikosi vya Burundi.

Burundi Pierre Nkurunziza
Rais Pierre NkurunzizaPicha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Andre Ndimurukundo amekuwa akimtafuta kakake Pascal tangu alipokamatwa na wakala wa ujasusi anayejulikana Desemba mwaka uliopita kwa madai alikuwa ameshiriki maandamano ya kumpinga Rais Nkurunziza.

"Tumekuwa tukivitembelea vituo vyote vya polisi tangu kukamatwa kwa Pascal lakina bila bahati na hatujui kama bado yuko hai," alisema Ndimurukundo, aliyekimbilia uhamishoni. "Lakini mwezi mmoja baada ya kukamatwa kwake, tulipokea taarifa za kushangaza kutoka kwa watu waliosema kaka yetu huenda akaachiwa kama tutalipa fedha, lakini tulifahamu hata tukilipa fedha hizo watekaji nyara wake hawangemuachia." Pascal, ambaye alikuwa na mke na watoto wanne, sasa anadhaniwa alikufa.

Wakili maarufu na mwanaharakati wa Burundi, Lambert Nigarura, amesema kundi la mawakili nchini humo limekuwa likijaribu kukusanya ushahidi kutoka kwa familia ambazo jamaa zao walipotea, kwa matumaini ya kuwashitaki baadhi ya maafisa wa serikali katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC, mjini The Hague.

"Changamoto kubwa inayotukabili ni kwamba familia hizi zinatishwa zisizungumze na serikali," alisema Nigarura. "Ulimwengu umewavunja moyo watu wa Burundi. Tunafanya kazi chini ya kitisho kikubwa kuwafichua wale walioua na hatimaye wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria."

Mwandishi: Josephat Charo/ape

Mhariri: Grace Patrica Kabogo