Burundi, Rwanda zaanza mazungumzo kurejesha mahusiano
26 Agosti 2020Mazungumzo hayo yaliyosimamiwa na Idara ya Usalama ya Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) yalifanyika kwenye mpaka wa Nemba ulioko mashariki mwa Rwanda kwenye eneo ambalo halimilikiwi na Rwanda wala Burundi.
Ulikuwa mkutano ulioukutanisha ujumbe mzito kutoka kila upande huku maafisa wa idara ya ujasusi kutoka pande hizo tatu - Rwanda, Burundi na ICGLR - ukitangaza mtazamo wake juu ya mkutano huo wa kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitano tokea nchi mbili hizo zilipoingia kwenye mzozo wa kidiplomasia.
Mkuu wa ujumbe wa Rwanda, Brigedia Jenerali Vincent Nyakarundi, alisema nchi yake "inathamini nafasi ya ICGLR katika kutatua mizozo, na kujituma kwa wajumbe wake ambao hufanya kila jitihada za kurejesha usalama kwenye eneo hili la maziwa makuu na siku zote kupambana ili hali ya ujirani mwema na kuaminiana kwenye mataifa hayo iendelee kuwepo."
"Hii ndiyo sababu kuu yetu sote kukutana hapa hii leo na namini baada ya mkutano huu, wote tutakuwa tumekwishatambua chanzo cha ukosefu wa amani unaosababishwa na makundi yenye silaha ya CRND na FNL yanayoisumbua Rwanda kupitia msitu wa Kibira upande wa Burundi.'' Alisema Nyakarundi, ambaye pia ni mkuu wa idara ya ujasusi kwenye jeshi la Rwanda.
Burundi yataka ushirikiano urudi
Kwa upande wake, mkuu wa ujumbe wa Burundi, Kanali Ernest Musaba, alisema hali mbaya iliyopo ilikuwa ikichochewa pia na hali ya usalama kwenye eneo la mashariki mwa DRC, hususan katika mpaka unaozitenganisha nchi za Rwanda na Burundi, ambayo si nzuri.
"Mkutano huu kwa hiyo ni fursa nzuri kwetu sote kuzungumza kwa uwazi juu ya sababu zinazochangia usalama huo mdogo na tunaamini kuwa hakutakuwepo na upendeleo wowote, ili ukweli uweze kujulikana na hatimaye sheria ichukue mkondo wake," alisema Musaba ambaye naye pia ni mkuu wa idara ya ujasusi kwenye jeshi la Burundi.
Mwakilishi kutoka idara ya ujasusi katika jumuiya ya ICGLR inayoyaunganisha mataifa 12 ya ukanda wa Maziwa Makuu, Kanali Leon Mahoungou, alizishauri pande hizo kuzidi kujongeleana karibu na kushirikiana kwa maslahi ya kila mmoja.
''Nia ya mkutano wa leo ni kutaka kujua kiini cha kuendelea kuwepo na mashambulizi yanayovuka mipaka, na wakati huo huo tutafute suluhisho la kukomesha kuzorota kwa usalama. Naamini kwa utashi wenu tutapata suluhu la kurejesha ushirikiano na uhusiano wa mataifa yenu, lakini kwa namna ya kipekee uhusiano wa majeshi yenu.''
Mkutano huo ulifanyika zikiwa zimepita wiki tatu baada ya Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi kutangaza kwamba nchi yake haikuwa tayari kuzungumza na nchi aliyoitaja kama ya wanafiki katika kile kilichoonekana kama kumjibu mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, aliyekuwa amependekeza mzozo huu uishe ili wananchi wa nchi hizo mbili warejee kwenye uhusiano wa kawaida.
Ripoti ya Sylvanus Karemera/DW Kigali