Burkina Faso yasitisha shughuli za vyombo viwili vya habari
26 Aprili 2024Mamlaka ya Burkina Faso imesema imesimamisha kwa wiki mbili matangazo ya redio ya Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC Africa na lile la Marekani la Voice of America, VOA, baada ya kuiangazia ripoti ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) iliyodai jeshi la nchi hiyo linatekeleza mauaji ya kiholela.
Ripoti hiyo ya Human Rights Watch ilidai nchi hiyo ya Afrika Magharibi ilifanya mauaji ya wanavijiji 223 wakiwemo watoto 56 mwezi Februari kama sehemu ya kampeni dhidi ya raia wanaotuhumiwa kushirikiana na makundi ya wanamgambo. Shirika hilo limesema mamlaka ya Burkina Faso imetekeleza mauaji hayo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Nchi hiyo imesema ripoti hiyo ina nia ya kuunyumbisha usalama na ndio maana ikasimamisha shughuli za vyombo hivyo vya habari kwa kuitangaza. Shughuli zao za mitandaoni nchini humo zikiwemo pia zile za HRW zimesitishwa.