Burkina Faso kukabiliwa na hali tete zaidi?
25 Januari 2022Vuguvugu la Wazalendo la MPSR ambalo limekusanya vikosi vyote vya ulinzi na usalama limeamua jumatatu hii usiku, kuupindua utawala wa Rais Marc Roch Christian Kaboré. Taarifa hiyo ilitolewa kwenye televisheni ya umma na mkuu wa jeshi Kader Ouedraogo, akiwa amezungukwa na askari wapatao kumi na tano.
Soma Zaidi: Burkina Faso: Milio mikubwa ya bunduki yarindima kwenye kambi kadhaa za jeshi
Kutokana na mapinduzi hayo, mipaka ya ardhi na anga imefungwa kuanzia usiku wa manane, serikali na Bunge vimevunjwa na katiba kusitishwa. Amri ya kutotoka nje imewekwa kuanzia saa tatu usiku hadi kumi na moja alfajiri.
Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imetiwa saini na kiongozi wa MPSR Luteni-Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba ambaye anaibuka kama shujaa mpya wa nchi hiyo.
MPSR imesema itapendekeza kwa muda mwafaka, ratiba ya kurejea kwa utaratibu wa kikatiba unaokubaliwa na wote. Lakini pia wametetea hatua yao ya mapinduzi.
Amesema, "Hatua iliyochukuliwa kwa lengo pekee la kuiwezesha nchi yetu iweze kurejea katika muelekeo bora na kuunganisha nguvu zetu zote ili kupigania uhuru wake na kujikwamua."
Hata hivyo baadhi ya raia wametaja kuunga mkono mapinduzi hayo kutokana kwamba walichoshwa na utawala uliopinduliwa ambao uliwanyima haki zao za msingi huku wakitarajia mema kwa utawala huu wa mpito na ule ujao.
"Nilikipigia kura chama cha MPP na sijutii hilo lakini tulivyoahidiwa sivyo vilivyotendeka, asilimia kubwa ya raia wa Burkina Faso walichoshwa na tunaweza kusema ni mapinduzi ya kupongezwa...Watu walichoshwa, uhuru wetu ulikandamizwa mno, tulijaribu na serikali hiyo bila mafaanikio, tutajaribu na hawa...muda wote ni mapinduzi, sisi hatupendi hayo, tunapenda amani, tunatarajia mambo mapya ambayo yataweza kuindeleza nchi." Amesema.
Marc Roch Christian Kaboré anapinduliwa miaka miwili baada ya kuchaguliwa tena kuiongoza Burkina faso kwa muhula mwengine wa miaka 5.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikaali mapinduzi hayo na kutoa wito kwa askari kuweka chini silaha zao na kulinda afya ya Rais aliepinduliwa.
Marekani imetoa wito kwa jeshi la Burkina Faso kumwachilia huru mara moja Rais Roch Marc Kaboré na kuheshimu Katiba na viongozi waliochaguliwa na raia wa nchi hiyo.
Vuguvugu la MPSR lililohusika na mapinduzi hayo limetoa wito kwa wazalendo, Waafrika waaminifu na marafiki wote wa Burkina Faso kuwaunga mkono na kushirikiana nao katika hatua hii muhimu ya mabadiliko katika historia ya nchi hiyo.
Soma Zaidi: Hali Burkina Faso inatia wasiwasi
Bakari Ubena