1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Burhan aonekana kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita

24 Agosti 2023

Kiongozi wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ameonekana katika video nje ya uwanja wa kamandi ya kijeshi mjini Khartoum kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

https://p.dw.com/p/4VX0x
Mkuu wa jeshi la Sudan jenerali Abdel Fattah Al-Burhan katika video iliyochapishwa katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook wa jeshi la Sudan mnamo Agosti 14, 2023
Mkuu wa jeshi la Sudan jenerali Abdel Fattah Al-BurhanPicha: Sudanese Army/AFP

Jeshi linasema ilichukuliwa video hiyo katika kambi ya jeshi la anga ya Wadi Sayidna huko Omdurman ng'ambo ya mto Nile kutoka mji mkuu Khartoum. Burhan amewaambia wanajeshi hao kwamba kazi wanayofanya inapaswa kuwahakikishia watu kwamba jeshi hilo lina wapiganaji na kwamba Sudan inalindwa na jeshi. Hata hivyo haikuwa wazi jinsi Burhan alivyoweza kuondoka Khartoum.

Soma pia: Wanamgambo wa Sudan wanyooshewa kidole kwa uovu

Dagalo amekuwa akimdhihaki Burhan 

Mara nyingi, mkuu wa kikosi cha dharura cha RSF Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, amekuwa akimdhihaki Burhan katika kile alichokitaja kuwa kujificha katika handaki, ijapokuwa Dagalo ameonekana tu mara moja kwa njia ya video mwezi uliopita, tangu kuanza kwa vita hivyo wakati alipokuwa akizungumza na wapiganaji wake nje ya nyumba katika eneo ambalo halikutambulishwa.

Umoja wa Mataifa watoa wito wa ufadhili wa kibinadamu

Huku mapigano hayo yakiwa tayari yamesababisha mzozo wa kibinadamu, Umoja wa Mataifa ulisema Jumatano (23.08.2023) kwamba mripuko wa ugonjwa wa Surua umeripotiwa pamoja na ongezeko la visa vya kuharisha, malaria na homa ya dengue.

Kiongozi wa RSF Mohammed Hamdan Dagalo akipiga saluti wakati wa mkutano katika eneo la Galawee, Kaskazini mwa Sudan mnamo mwezi Juni 15, 2019 wakati akihudumu kama naibu mkuu wa baraza la kijeshi la Sudan
Kiongozi wa RSF Mohammed Hamdan DagaloPicha: AP/picture alliance

Mamadou Dian Balde, mkurugenzi wa ofisi ya kanda ya Mashariki na pembe ya Afrika na maziwa makuu ambaye pia ni mratibu wa kikanda wa wakimbizi wa shirika la UNHCR kwa hali ya Sudan amesema kuwa wanaposaidia na kujaribu kushughulika mahitaji ya kimsingi kuhusu chakula, afya, lishe bora tayari wanaona mapungufu makubwa na kutoa wito wa ufadhili mkubwa wa maendeleo kusaidia mifumo yao.

Soma pia: Karibu watoto 500 wamefariki kutokana na njaa Sudan

Wapiganaji wa RSF wapambana na jeshi la nchi kwa siku ya nne mfululizo

Katika hatua nyingine, kwa siku ya nne mfululizo Jumatano (23.08.2023) wapiganaji wa kikosi cha RSF walipigana na jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum kudhibiti kambi kuu ya kijeshi katika eneo la Kusini mwa mji huo. Wapiganaji hao walianza mashambulizi yao kwenye eneo hilo kubwa kimkakati siku ya Jumapili. Wakazi wa Al-Shajara, mtaa jirani na kambi hiyo, waliripoti hasara kubwa kwa pande zote mbili katika siku ya kwanza ya mashambulizi hayo wakati mapigano yalifanyika mfululizo.

Tazama pia: 

Mmoja wa wakaazi hao anasema kuwa hayo ndiyo mapigano ya muda mrefu zaidi katika eneo hilo.

Jeshi la nchi hiyo likiongozwa na Burhan limetoa taarifa kadhaa na video likisema kuwa limezuia mashambulizi ya RSF, lakini kikosi hicho kimesema kuwa tangu mapema jana, kimechukuwa udhibiti wa karibu kambi yote huku maeneo kidogo yakiwa bado yanawaniwa.