1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ulaya lamtambua Gonzalez rais halali Venezuela

20 Septemba 2024

Bunge la Ulaya limepitisha hapo jana azimio la kumtambua mgombea wa upinzani wa Venezuela Edmundo Gonzalez Urrutia kuwa rais halali wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4ktW6
 Edmundo Gonzalez anayedai kushinda uchaguzi wa Venezuela.
Edmundo Gonzalez anayedai kushinda uchaguzi wa Venezuela.Picha: Ariana Cubillos/AP Photo/picture alliance

Bunge hilo limesema pia kuwa viongozi wa Ulaya wanatakiwa kufanya kila liwezekanalo ili kumuwezesha kuchukua madaraka ifikapo Januari 10 mwakani.

Kura hiyo iliyopingwa na vyama vya mrengo wa kushoto ilipitishwa kwa kura 309 dhidi ya 201 na iliwezeshwa kutokana na muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia.

Soma zaidi: Kwa namna gani Bunge la Ulaya linasaidia kuhalalisha mrengo wa kulia?

Hata hivyo, maamuzi ya kura hiyo si ya lazima kutekelezwa na serikali za mataifa wanachama na hayaakisi msimamo wa nchi za Umoja wa Ulaya.

Gonzalez Urrutia mwenye umri wa miaka 75, ambaye alikimbilia nchini Uhispania, anadai kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais wa Julai huku rais aliye madarakani, Nicolas Maduro, akidai pia kuwa alishinda muhula wa tatu wa miaka sita katika uchaguzi uliogubikwa na utata.