Bunge la Uingereza laitambua Palestina
14 Oktoba 2014Wabunge 274 waliipigia kura ya ndio hoja iliyowasilishwa na mbunge wa chama cha upinzani cha Labour, Grahame Morris, ambayo inaitaka serikali iitambue Palestina sambaba na taifa la Israel, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupatikana suluhisho la kuwapo kwa mataifa hayo mawili. Ni kura 12 tu ndizo zilizokataa pendekezo hilo.
"Kura za ndiyo upande wa kulia ni 274, kura za hapana upande wa kushoto ni 12. Na ndiyo wameshinda. Ndiyo wameshinda. Natangaza rasmi suala kuu kama lilivyorekebishwa limekubalika," Spika wa Bunge John Bercow alithibitisha matokeo hayo.
Hata hivyo, kura hiyo haiilazimishi serikali ya Waziri Mkuu David Cameron, kubadili sera yake kuelekea mzozo huo mkongwe wa Mashariki ya Kati, ambao kihistoria ulianzishwa na Himaya ya Uingereza. Lakini mbunge Grahame Morris aliyewasilisha azimio hilo, alimtolea wito Cameron na serikali yake kuakisi uamuzi wa bunge na hivyo kuitambua rasmi Palestina.
"Ni nadra sana kwa bunge kuzungumza kwa kauli moja, kama lilivyofanya leo, na ningependa kumshauri waziri kwa mtazamo wa kila kilichosemwa hapa, kwamba hii ndiyo dhamira ya bunge, na kwamba ni kitu sahihi kuitambua Palestina, na natazamia kuwa atatekeleza hilo." Alisema Morris bungeni.
Serikali haijabadili sera yake
Waziri anayehusika na masuala ya Mashariki wa Kati, Tobias Ellwood, alisema Uingereza itaitambua Palestina kama dola pale tu hatua itakaposaidia kuleta amani.
Kabla ya kura hiyo kupigwa, msemaji wa ofisi ya waziri mkuu, alisema Uingereza itaendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa, zikiwemo Israel na Mamlaka ya Palestina, kuunga mkono suluhisho la madola mawili huru. Waziri Mkuu na wajumbe wa baraza lake la mawaziri walijiepusha na kura hiyo.
Aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wakati wa Tony Blair, Jack Straw, aliliambia bunge kuwa shinikizo ndiyo lugha pekee inayotambuliwa na utawala wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na hivyo azimio hilo litaongeza uzito kwenye shinikizo la kimataifa la kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati.
Israel yapinga
Tayari Israel, kupitia wizara yake ya mambo ya nje, imetoa taarifa ya kulilaani azimio hilo, ikisema linahujumu uwezekano wa kupatikana kwa amani ya kudumu.
"Kutambuliwa Palestina na jumuiya ya kimataifa katika wakati usio muafaka kunatuma ujumbe kwa uongozi wa Palestina kwamba unaweza kukwepa kufanya maamuzi magumu yanayopaswa kufanywa na pande zote mbili," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Israel.
Mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, alisema serikali yake italitambua taifa la Palestina, tangazo ambalo nalo liliibua pongezi kutoka kwa Wapalestina na lawama kutoka Israel.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters
Mhariri: Oummilkheir Hamidou