Bunge la Colombia laidhinisha makubaliano ya amani
Taarifa kutoka bunge zimesema makubaliano hayo yaliyofanyiwa mageuzi kadhaa yameidhinishwa kwa kura 130 kwa sufuri baada ya Baraza la seneti hapo jana pia kupiga kura kwa kauli moja kuyaidhinisha.
Rais wa Colombia Juan Manuel dos Santos amesema wapiganaji wa FARC wapatao 7,000 sharti waanze kuondoka kutoka ngome zao kuelekea maeneo yanayotajwa ya amani katika kipindi cha siku tano zijazo kuanzia leo na kuongeza shughuli ya kuwapokonya silaha itaanza katika kipindi cha siku thelathini zijazo.
Baada ya miaka 52 ya vita, zaidi ya miaka minne ya mazungumzo na sherehe mbili ya kutiwa saini makubaliano, kuridhia kwa mabunge yote mawili kwa makubaliano hayo ya amani kunawaruhusu waasi wa FARC kuweka chini silaha na kujiunga na siasa.
Miezi michache iliyopita makubaliano hayo yalishindwa kutekelezwa baada ya wapiga kura kuyapoinga katika kura ya maoni. Rais dos Santos amesema hakutakuwa na kura nyingine ya maoni.
Mzozo huo wa Colombia umesababisha vifo vya zaidi ya watu 220,00 na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao. Serikali ya Colombia inakadiria kuwa mzozo huo wa muda mrefu zaidi katika kanda ya Amerika ya Kusini umewaathiri zaidi ya watu milioni 7.6.
Mwandishi: Caro Robi//Afp/Reuters