Bunge la Catalonia kumchagua kiongozi mpya bila Puigdemont
8 Agosti 2024Puigdemont alikaidi waranti wa kukamatwa na akarejea Uhispania mapema leo baada ya kuwa mafichoni kwa miaka saba.
Kiongozi huyo ambaye anasakwa kuhusiana na jaribio lililoshindwa la uhuru wa Catalonia mwaka wa 2017, aliwahutubia maelfu ya wafuasi wake mapema leo katika bustani iliyoko karibu na bunge. Aliwaambia amerejea kuwakumbusha kuwa bado yupo.
"Licha ya jitihada zao, licha ya kutaka kutuumiza kabisa, licha ya kuwa wameona sura yao ya kandamizi, leo tumekuja hapa kuwakumbusha kuwa bado tupo! Bado tuko hapa! Na bado tuko hapa kwa sababu hatuna haki ya kukata tamaa." alisema mwanasiasa huyo.
Puigdemont aliwasili Barcelona akitokea Ubelgiji ambako amekuwa akiishi uhamishoni.
Kura ya maoni aliyoiandaa mwaka wa 2017 ya kudai uhuru wa Catalonia, ilitangazwa kuwa kinyume cha sheria kwa wakati huo na serikali kuu ya Uhispania na Mahakama ya Kikatiba.