Bunduki yatawala kusini mashariki mwa CAR
8 Agosti 2014Eneo la Upper M'bomou linalopatikana kati ya Sudan kusini na Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, lilishuhudia upinzani mdogo wa waasi wa kundi la Seleka kati ya mwaka 2012 na 2013, walionyakua madaraka katika mji mkuu Bangui na kudhibiti mamlaka kwa miezi 10. Eneo hilo pia limekwepa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na wanamgambo wa kikristo wa anti Balaka, lakini utawala wa mtutu wa bunduki ndio unaoshuhudiwa.
"Hakukuonekana vikosi vya Seleka hapa. Tangu kuanza mashambulizi mwishoni mwa mwaka 2012 mpaka walipouteka mji mkuu Bangui na baadaye kulazimishwa kuondoka madarakani, hakuna hata mmoja aliyejaribu kushambulia maeneo haya," amesema Blaise Mboligani, mkaazi wa mji mkuu wa eneo hilo, Obo. "Wanajua wakifanya hivyo watakabiliana na wapiganaji wanaume walio ngangari kuliko hao," akaongeza kusema mkaazi huyo.
Wanajeshi kadhaa wa mataifa ya kigeni wana kambi zao katika eneo hilo, wakiwemo wanajeshi kutoka Uganda, wanaoungwa mkono na wanajeshi wa Marekani, ambao tangu mwaka 2009 wamekuwa wakisaidia kumsaka kiongozi wa kundi la waasi wa Lords Resistance Army, LRA, Joseph Kony. Baada ya kufurushwa kutoka Uganda, wapiganaji wa LRA sasa wanapatikana katika eneo la msitu la Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Seleka hawafiki kusini mashariki
Kwa mujibu wa afisa wa polisi katika mji wa Bangassou, wapiganaji 15 wa Seleka waliokuwa wamejaribu kwenda katika eneo hilo mapema mwezi Julai mwaka huu baada ya kuingia wilaya ya M'bomou, walipigwa risasi na wanajeshi wa Uganda waliowadhania kuwa ni wapiganaji wa kundi la LRA. Afisa huyo pia amesema baada ya makabiliano makali mjini Nzako, wapiganaji wa Seleka waliobaki walikimbia na kuacha vifaa vyao, bunduki, nguo na vitatu.
Jeshi la Uganda liliruhusiwa kuwasaka waasi wa LRA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo mwaka 2009 na rais wa zamani wa nchi hiyo, Francoise Bozize, aliyepinduliwa madarakani mwezi Machi mwaka uliopita na waasi wa Seleka. Vikosi maalumu vya Marekani vilivyowasili miaka miwili baadaye pia vilijikita katika kuwasaka waasi hao wa Uganda.
Zaidi ya wanajeshi 7,000 wametumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kama sehemu ya operesheni ya Ufaransa, Sangaris, na tume ya Umoja wa Afrika, kujaribu kukomesha umwagaji damu wa kikabila katika taifa hilo. Hakuna mwanajeshi hata mmoja aliyewahi kupelekwa katika eneo la kusni mashariki, ingawa vikosi vimewekwa katika maeneo mengine ya nchi hiyo masikini katika jitihada za kuyatuliza machafuko.
Lakini waasi wa Seleka walipolichakaza jeshi la nchi hiyo ambalo halikuwa limepewa mafunzo mazuri, waliwafungulia mlango pia wawindaji haramu wa wanyamapori na majangili kuendesha shughuli zao katika eneo hilo la kusini mashariki lenye misitu mikubwa. Umoja wa Mataifa unasema waasi wa LRA hufadhili shughuli zao kwa biashara haramu ya pembe za ndovu zinazouzwa katika soko linaloendelea kunawiri barani Asia.
Kiongozi wa kidini katika mji wa Obo amesema hawaelewi lolote kuhusu balaa hilo na kwamba wanajeshi wa Mareknai na Uganda wana uwezo wa kuwaangamiza wawindaji wote haramu katika eneo hilo, lakini wanawaachia waendelee. Kiongozi huyo aidha amesema uamuzi huo wa kutowachukulia hatua umesababisha athari kubwa miongoni mwa wakaazi wa mji wa M'bomou pamoja na wanyamapori.
Athari za ujangili ni mbaya
Afisa mmoja wa jeshi amethibitisha athari za ujangili zimefikia pabaya. Amesema wawindaji haramu huenda katika eneo hilo katika makundi yanayopishana, wakitumia mipaka ambayo haina usalama imara na mzozo ambao umevivuruga kabisa vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuua kiholela wanyamapori waliobakia.
Wakisaidiwa na wakaazi ambao hufanya kazi ya kuwafuatilia wanyama, wawindaji hao huua tembo, simba, vifaru na kasa. Baadhi ya wawindaji hao wamelihama eneo hilo kuelekea upande wa magharibi kuwatafuta wanyama waliokimbilia huko wanaolindwa kwa sababu wanakabiliwa na kitisho cha kutoweka.
Pamoja na wawindaji haramu, wafanyabiashara wa madini ya almasi na dhahabu pia wamefurika katika eneo hilo. Afisa huyo wa jeshi amesema aneo la kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati limekuwa eneo lisilo na utawala wa kisheria; watu huingia kutoka nchini Chad na Sudan ambao hufanya wanachokitaka na kisha kuondoka. Afisa huyo amesema anaamini madini ya vito na raslimali za madini zinasafirishwa nje ya taifa hilo.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE
Mhariri: Saumu Yusuf