Bundestag yapinga kuipatia Ukraine makombora ya Taurus
22 Februari 2024Wabunge 182 tu walioipigia kura hoja hiyo, wakati 480 wakiipinga huku watano wakijizuia kupiga kura. Hoja hii ya kutuma makombora hayo nchini Ukraine iliwasilishwa na muungano wa vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kulia vya Christian Democtaric Union (CDU) na Christian Social Union (CSU).
Kabla ya kura hiyo, kiongozi wa upinzani Friedrich Merz aliwasihi wabunge wa muungano wa vyama tawala kuiunga mkono hoja hiyo. Muungano huo badala yake umewasilisha hoja yao ya pamoja ya kutoa wito wa kupelekwa kwa mifumo zaidi ya makombora ya masafa marefu pamoja na risasi nchini Ukraine, bila ya kuyataja kwa uwazi makombora ya Taurus.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani alihutubia Bunge
Katika hotuba yake mbele ya wabunge wa Bundestag, Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius aliepuka kutaja neno la "Taurus", lakini akasisitiza kuhusu kuiunga mkono Ukraine, akisema uchokozi wa jeshi la Urusi dhidi ya Ukraine si hatari kwa uhuru wa Ukraine pekee bali pia utakuwa na matokeo katika mustakabali wa Ujerumani na Ulaya.
Soma pia: Kansela Olaf Scholz akataa kutoa makombora ya Taurus kwa Ukraine
Pistorius ambaye ni mwanachama wa chama cha mrengo wa kushoto cha Kansela Olaf Scholz cha Social Democratic Party (SPD), amesisitiza haja ya kuongeza matumizi ya ulinzi kwa muda mrefu na kuhakikisha kuwa jeshi la Ujerumani limejitayarisha na kuwa na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mapambano na kujihami dhidi ya vitisho vya usalama wa taifa.
Viongozi wa Ukraine walikuwa na matumaini makubwa
Uamuzi huu wa Bunge la Ujerumani la Bundestag ni pigo kwa serikali mjini Kyiv ambayo imekuwa ikiitaka Ujerumani kuipatia makombora hayo ya kisasa ili kuongeza uwezo wake wa kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Soma pia:Ukraine yaihimiza Ujerumani kuipatia makombora ya Taurus
Viongozi wa Ukraine wamekuwa wakiitaka Ujerumani na washirika wengine wa kimataifa kuipatia Kyiv silaha na mifumo ya ulinzi wa anga, hasa silaha za masafa marefu.
Siku ya Alhamisi, Meya wa jiji la Kyiv Vitali Klitschko alikuwa na matumaini na alisema hatimaye sasa ni wakati wa Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani kutuma makombora hayo ya Taurus nchini Ukraine.
(Vyanzo: dpa,dw)