1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yaingia mapumziko ya wiki mbili

20 Desemba 2021

Bundesliga imekwenda mapumziko mafupi ya msimu wa baridi. Na baada ya kupigwa mechi 17 kati ya 34, vinara Bayern Munich wameelekea mapumziko ya wiki mbili wakiwa mabingwa wa mapukutiko.

https://p.dw.com/p/44aWU
Fußball Bundesliga | Bayern München - VfL Wolfsburg
Picha: Alexander Hassenstein/Getty Images

Miamba hao wa Bavaria wapo kwenye mkondo wa kushinda taji la 10 la Bundesliga mfululizo baada ya ushindi wa 4 – 0 dhidi ya Wolfsburg. Wameweka mwanya wa pointi tisa dhidi ya nambari mbili Borussia Dortmund ambao walipoteza nafasi ya kuwakaribia jana walipoduwazwa na Hertha Berlin kwa kufungwa mabao 3-2.

Freiburg inaingia mapumziko ikiwa katika nafasi ya tatu na pengo la pointi 14 dhidi ya vinara Bayern baada ya kuiondoa kwenye nafasi hiyo Bayer Leverkusen kwa kuwapiga 2 – 1. Ni nafasi ya juu zaidi ya mzunguko wa kwanza wa ligi katika historia ya klabu hiyo

Katika mechi nyingine ya jana Antony Modeste aliiokoa Cologne na kuipa ushindi wa 1- 0 dhidi ya Stuttgart zikiwa zimesalia dakika mbili mechi kuisha. Ushindi huo umeinyanyua Cologne hadi nafasi ya nane wakati Stuttgart wakishuka katika nafasi ya timu tatu za mkia. Bundesliga itarejea Januari saba.

Hatumhitaji Halaand: Hainer

Fußball Bundesliga | Dortmund vs Mainz | Tor Haaland
Haaland anaweza kuondoka Dortmund msimu ujaoPicha: INA FASSBENDER/AFP/Getty Images

Rais wa Bayern Munich Herbert Hainer amefuta uwezekano wa kutuma ofa ya kumsajili mshambuliaji wa Dortmund Erling Haaland na anatumai kuwa mshambuliaji wao anayevunja rekodi kila kukicha Rpbert Lewandowski atatundika daluga dimbani Allianz Arena.

Halaand, mwenye umri wa miaka 21 yuko na mkataba na Dortmund hadi 2024, lakini anaweza kuondoka mwaka ujao wakati kipengele cha kumruhusu kufanya hivyo kitakapohalalishwa. Inaripotiwa ni cha euro milioni 80.

Mino Raiola, wakala wa Halaanda, hivi karibuni alisema kuna fursa kubwa kuwa Erling ataondoka mwishoni mwa msimu, akizitaja Bayern, Real Madrid, Barcelona na Manchester City kama vilabu anavyoweza kutua. Lakini Hainer ameweka wazi kuwa Bayern wanafuraha kubwa kuw a na Lewandowski, ambaye alijiunga nao kwa usajili huru kutoka Dortmund mwaka wa 2014.

Morway huyo amefunga mabao 76 katika mechi 75 tangu Januari 2020.

Lewandowski wa mabao mengi katika Bundesliga msimu huu akiwa na 19 na ametikisa nyavu mara 324 katika mechi 354 za Bayern.

Alifunga bao Ijumaa katika ushindi wao wa 4 – 0 dhidi ya Wolfsburg na kuweka rekodi mpya ya mabao 43 ya Bundesliga katika mwaka mmoja. Ni mara ya pili mwaka huu kuvunja rekodi y amuda mrefu ya nguli wa Bayern Gerd Mueller baada ya Lewa kumaliza msimu wa 2020/21 na rekodi mpya ya mabao 41 ya ligi.

AFP, Reuters, DPA