BUECHENBACH : Wazee wa Ujerumani waupanda Mlima Kilimanjaro
3 Oktoba 2005Kundi la wazee 19 wa Ujerumani akiwemo mmoja mwenye nyonga ya bandia wameupanda mlima mrefu kabisa barani Afrika Kilimanjaro baada ya kumaliza mazoezi magumu ya mafunzo.
Wastaafu hao wenye umri kati ya miaka 60 na 70 wameweza kupanda hadi mita 6,000 za Mlima Kilimanjaro nchini Tanzania kwa msaada wa mpanda mlima mkongwe Hubert Schwarz.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa kusini mwa Ujerumani Shwarz ambaye pia alikuwa mkufunzi wa wazee hao amesema ni jambo la kustaajabisha jinsi wazee hao walivyoonyesha ushupavu na nia katika changamoto hiyo.
Kundi hilo ambalo wengi wao wakiwa ni wanagenzi wa kupanda milima walikuwa katika mafunzo kwa wiki kadhaa ya kupunguza uzito na kujenga nguvu huku mpangilio wao wa kula ukiwa chini ya taratibu kali.