1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bouteflika: Nitaitisha uchaguzi wa mapema nikichaguliwa

4 Machi 2019

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ameahidi kwamba hatahudumu kwa muhula kamili iwapo atachaguliwa tena kama rais katika uchaguzi wa mwezi Aprili, baada ya maandamano makubwa kufanyika nchini humo.

https://p.dw.com/p/3EOzQ
Algerien | Präsident Abdelaziz Bouteflika
Picha: Reuters/R. Boudina

Maandamano hayo yalikuwa yanapinga harakati zake za kuongeza muda kwenye miaka ishirini aliyotawala. Kituo cha televisheni cha Ennahar kinasema kuwa ameahidi kuachia ngazi baada ya mwaka mmoja iwapo atachaguliwa.

Tangazo hilo lililosomwa kwa niaba yake na mkurugenzi wake wa kampeni Abdelghani Zaalane lilisema rais huyo amepanga kuandaa uchaguzi mpya mapema.

Mkurugenzi wa kampeni aliwasilisha nyaraka baada ya tangazo

"Uchaguzi mpya wa urais utafanyika tena ambao utatokana na mkutano wa kitaifa tutakaofanya. Naahidi sitagombea tena urais katika uchaguzi huo," alisema Abdelghane, "lengo la uchaguzi huo ni kuhakikisha makabidhiano ya madaraka kwa njia ya amani namazingira yaliyo huru na wazi. Mkutano huo wa kitaifa ndio utakaoamua tarehe ya uchaguzi," aliongeza mkurugenzi huyo.

Algerien Proteste gegen Verlängerung der Amtszeit von Präsident Abdelaziz Bouteflika
Waandamanaji wakiandamana dhidi ya hatua ya Bouteflika kuwania urais tenaPicha: picture alliance/AA/F. Batiche

Mara tu baada ya tangazo hilo kutolewa mkurugenzi huyo wa kampeni aliwasilisha nyaraka zake za kugombea kiti hicho katika uchaguzi wa Aprili 18 kuelekea muda wa mwisho wa kuwasilisha nyaraka hizo uliokuwa umewekwa wa saa sita usiku wa jana Jumapili. Kabla tangazo hilo mkuu wa tume ya uchaguzi Abdelwahab Derbal alisema wagombea woteni sharti wawasilishe nyaraka zao binafsi, kwa hiyo iwapo hilo litazingatiwa basi huenda Bouteflika asiruhusiwe kugombea.

Barua hiyo ya Bouteflika huenda ikaonekana kama mbinu ya kutaka kuwaridhisha wale walioandamana kwa siku kumi kupinga hatua yake ya kugombea tena uongozi wa nchi hiyo.

Kulizuka maandamano mengine ya kuipinga serikali muda mfupi baada ya tangazo hilo kutolewa huku mamia ya vijana wakiandamana katika mitaa ya Mji Mkuu wa Algiers usiku ambapo polisi walikuwa wamefunga barabara. Maandamano hayo lakini yanadaiwa kwamba yalikuwa ya amani. Djamel Marniche ni mmoja wa walioshiriki maandamano hayo.

"Tatizo ni mfumo. Yeye hataki kuondoka. Kwa hiyo tangu tupate uhuru mpaka sasa, wameifilisi nchi. Kwa sasa, vijana wa nchi hiyo wameamka na wanawataka waondoke madarakani," alisema Djamel.

Bouteflikla hana uhusiano mzuri na vijana wa Algeria

Taarifa hiyo ya Bouteflika ndiyo ya kwanza tangu maandamano yazuke siku kumi zilizopita, maandamano hayo yakiwa ndiyo makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Algeria tangu vuguvugu la mataifa ya Kiarabu mwaka 2011.

Algerien Protest gegen Abdulaziz Bouteflika
Muandamanaji akikabiliwa na maafisa wa polisi mjini AlgiersPicha: picture alliance/dpa

Kama ishara inayoonyesha uhusiano mbovu alio nao na vijana ambao ni wengi nchini humo, aliwasilisha ujumbe kupita njia ya barua kama alivyokuwa akifanya siku zote tangu augue kiharusi mwaka 2013.

Wapinzani wake wanasema hafai tena kuongoza kutokana na hali yake mbaya ya kiafya na kile wanachokiita ufisadi uliokita mizizi, pamoja na ukosefu wa mageuzi ya kiuchumi ili kukabiliana na kiasi kikubwa cha ukosefu wa ajira ambacho kinapindukia asilimia 25 kwa watu walio chini ya umri wa miaka 30.