Bouteflika apata pigo kutoka chama chake mwenyewe
25 Machi 2019Mpango wa rais mkongwe wa Algeria Abdelaziz Bouteflika wa kuitisha mkutano wa kitaifa kutafuta suluhu ya vuguvugu la maandamano ya upinzani, umekataliwa na chama chake mwenyewe.
Msemaji wa chama hicho, FLN alisema jana kupitia kituo cha televisheni cha Dzair News kinachomilikiwa na watu binafsi, kwamba mkutano huo hauna maana tena, kwa sababu ungewahusisha viongozi ambao hawakuchaguliwa, na tayari umekataliwa na waandamanaji.
Msemaji huyo, Hocine Khaldoun amesema suluhisho kwa matatizo ya kisiasa ya Algeria litamalizwa na uchaguzi, utakaomweka madarakani rais anayeweza kuzungumza na wananchi.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Bouteflika mwenye umri wa miaka 82, ambaye ameonekana hadharani kwa nadra sana tangu alipopata ugonjwa wa kiharusi mwaka 2013.
Kiongozi huyo ambaye alikabiliwa na maandamano ya mwezi mzima, alifuta uchaguzi uliotarajiwa kufanyika Aprili 18, na kuitisha mkutano wa kitaifa ambao ungewashirikisha wawakilishi wa makundi ya wananchi ili kuandaa uchaguzi mpya.