Bouteflika ambadilisha meneja wake wa kampeni ya urais
3 Machi 2019
Taarifa za uteuzi wa Abdelghani Zaalane zimekuja siku moja baada ya mamia kwa maelfu ya Walgeria kuandamana dhidi ya muhula mwingine wa urais kwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82, ambaye yuko nchini Uswisi kwa ukaguzi wa afya yake. Zaalane ni waziri.
Shirika la habari la APS halikutoa sababu yoyote kuhusiana na uamuzi huo wa Bouteflika kumbadilisha meneja wake wa hapo mwanzo Abdelmalek Sellal , ambaye alisema siku ya Jumanne kuwa rais atawasilisha nyaraka zake rasmi za uchaguzi leo Jumapili, muda wa mwisho wa kufanya hivyo kwa wagombea.
Wapinzani wanasema Bouteflika , ambaye aliugua kiharusi nmwaka 2013 na ameonekana hadharani mara chache tangu wakati huo, hawezi tena kuliongoza taifa hilo la Afrika kaskazini, mtoaji mkubwa wa mafuta na gesi.
Lakini katika ishara ya udhaifu kuweza kutoa changamoto ya kupambana dhidi ya chama tawal cha National Liberation Front FNL, muungano wa kundi la vyama vya upinzani kwa mara nyingine tena umemtaka Bouteflika kujiondoa lakini kundi hilo halijamteua mgombea wao.
Siku ya Ijumaa kulishuhudiwa kujitokeza kwa kundi kubwa kabisa kuwahi kuonekana la maandamano makubwa nchini Algeria linalopinga serikali tangu vuguvugu la maandamano ya umma katika mataifa ya Kiarabu miaka minane iliyopita. Bouteflika hajazungumzia moja kwa moja maandamano hayo.
Mpiganaji mkongwe
Kama wengi wa watu mashuhuri katika nchi hiyo iliyotoa viongozi wa FNL, maafisa wa jeshi na wafanyabiashara matajiri, Bouteflika ni mpiganaji mkongwe wa vita vya kuwania uhuru nchini Algeria dhidi ya Ufaransa kuanzia mwaka 1954-1962. Amekuwa madarakani tangu mwaka 1999.
Maafisa walisema wiki iliyopita kwamba atakwenda Geneva kwa kile ambacho hakikuwekwa wazi kuhusu uchunguzi wa afya yake.
Vyombo vya habari nchini Algeria havikuripoti kuhusu safari yake lakini televisheni ya umma ya Uswisi imesema jioni ya Jumamosi kwamba Bouteflika ameendelea kuwapo katika hospitali ya chuo kikuu mjini Geneva.
Jumla ya watu 183 walijeruhiwa katika maandamano ya Ijumaa nchini Algeria na mtu mmoja amefariki kutokana na mshituko wa moyo, limesema shirika la habari la APS.
Mji mkuu Algiers ulikuwa kimya jana Jumamosi na maduka yalifunguliwa.
Maandamano makubwa, ambayo ni nadra kuyaona nchini Algeria huku kukiwa na ulinzi mkali, dhidi ya hatua ya kuchaguliwa tena kwa Bouteflika yalianza wiki moja iliyopita na yameongezeka idadi ya washiriki.
Wengi wa Waalgeria wameepuka harakati za wazi za kisiasa kwa miaka kadhaa, wakihofia matatizo kutoka jeshi la usalama ama kuchoshwa na viongozi wa vita vya ukombozi ambao wameendelea kuiongoza nchi hiyo tangu uhuru.
Baada ya mapigano ya muongo mmoja ya kundi la Kiislamu ambayo Bouteflika aliyazima mapema katika utawala wake, Waalgeria mara kadhaa wamevumilia mfumo wa kisiasa unaokandamiza upinzani kama gharama wanayolipa kwa ajili ya amani na uthabiti.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Jacob Safari Bomani