Botswana kuwa mthibitishaji almasi zinazokwenda G7
28 Novemba 2024Botswana, ambayo ni mmoja ya wazalishaji wakubwa wa almasi barani Afrika, itaungana na Antwerp kama mthibitishaji wa chimbuko la almasi ghafi kwa ajili ya kusafirishwa katika mataIfa ya G7, yaliopiga marufuku uagizaji wa madini ya Urusi kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
Ushirikishwaji wa Botswana unalenga kushughulikia wasiwasi wa wazalishaji wa Afrika kuhusu usawa wa kiuchumi. Mfumo wa awali wa uthibitishaji ungeshuhudia almasi zote zikipitia kitovu cha almasi cha Ulaya mjini Antwerp kwa ajili ya uhakiki, kwa kutumia teknolojia mpya ya ufuatiliaji.
Lakini wazalishaji wa almasi wa Afrika, mataifa ya Angola, Botswana na Namibia, pamoja na kampuni ya uchimbaji ya De Beers, walisema mfumo huo haukuwa wa haki na kwamba ungeathiri uchumi wao.
Mfumo wa ufatiliaji ulipanswa kuanza kufanya kazi kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, lakini Umoja wa Ulaya ulichelewesha utekelezaji wake hadi Machi 2025.