Boti iliyowabeba Warohingya kuruhusiwa bandarini Indonesia
29 Desemba 2021Maafisa katika jimbo la Aceh, lililo magharibi mwa kisiwa cha Sumatra wamesema watawapa takriban abiria 120 waliokuwemo ndani ya chombo hicho cha baharini msaada wa chakula, dawa na maji, lakini hawatawaruhusu kutafuta hifadhi nchini Indonesia, licha ya miito na maombi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ikiitaka Indonesia kufanya hivyo.
Afisa katika wizara ya usalama ya Indonesia, Armed Wijaya amesema serikali ya Indonesia imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuwanusuru wakimbizi wa Rohingya waliokwama kwenye mashua karibu na wilaya ya Biereun kwenye jimbo la Aceh kutokana na kuzingatia misingi ya ubinadamu.
Afisa huyo ameongeza kusema kwamba uamuzi huo ulifanywa baada ya kuzingatia dharura hiyo na hali ambayo wakimbizi wanapitia ndani ya boti hiyo na kwamba abiria wake wengi walikuwa ni wanawake na watoto.
Wavuvi wawili walioshuhudia boti hiyo iliyokwama wamewaelezea waandishi wa habari wa shirika la Reuters kuwa chombo hicho kilikuwa katika hatari ya kuzama ndani ya siku chache zijazo.
Aditya Setiawan, mmoja kati ya wavuvi hao ameserma kulikuwa na sehemu mbili ambazo zilikuwa zinavuja kwenye boti hiyo na pia maji yalikuwa mengi. Katika ukanda wa video ulioangaliwa na waandishi wa habari wa Reuters, ulionesha watu wamejaa katika sehemu za juu na chini ya chombo hicho kilichotengenezwa kwa mbao.
Indonesia haijatia saini Mkataba wa mwaka 1951 wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi na mara nyingi ni nchi inayotumiwa na watu wanaosafiri kwenda kutafuta hifadhi kwenye nchi ya tatu.
Kamishna wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi (UNHCR) na shirika la Amnesty International waliitolea mwito serikali ya Indonesia iiruhusu mashua hiyo kutafuta hifadhi nchini mwake.
Wakimbizi ambao ni Waislamu wa jamii ya Rohingya kutoka Myanmar wamekuwa kwa miaka kadhaa sasa wakisafiri kwa vyombo vya baharini hasa katika miezi ya Aprili na Novemba wakati bahari huwa shwari na kufika katika nchi kama Malaysia, Thailand na Indonesia lakini wengi wa wakimbizi hao wamekuwa wakikataliwa kupewa hifadhi na kurudishwa walikotoka.
Chanzo:RTRE