Borussia Dortmund yaiadhibu FC Kolon kuifuata Hamburg
18 Septemba 2017Mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga Bayern Munich wameonesha kwamba wanania ya kurejea katika nafasi yao baada ya kuirarua Mainz 05 kwa mabao 4-0 wakiwa nyumbani , baada ya wiki iliyopita kuteleza na kubugia mabao 2-0 nyumbani kwa Hoffenheim. Kikosi cha kocha Carlo Ancelotti kilijisahihisha na kutoa jibu mjarabu baada ya wiki ya mtafaruku ndani ya klabu hiyo, ikiwa wachezaji mbali mbali nyota wakitoa matamshi ya kutatanisha kuhusu mahusiano yao na kocha na pia klabu hiyo.
Robert Lewandowski, Frank Ribery , Thomas Mueller na pia Arjen Robben walitoa maneno ya ama malalamiko ama kukosoa uongozi wa klabu. Licha ya mtafaruku huo wachezaji wa Bayern waliweza kuonesha uwanjani kwamba wao ni moto wa kuotea mbali na kuirarua Club Anderlecht ya Ubelgiji kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Champions League katikati ya wiki.
Mlinzi wa Bayern Mats Hummels alikuwa na haya ya kusema baada ya pambano dhidi ya Mainz 05.
"Nafikiri , tumeridhika na nmchezo wa leo. Bila shaka ilikuwa ni hatua tu katika njia sahihi. Lakini hata hivyo ilikuwa ni jibu la wazi , kwamba siku ya Jumanne hakuna kitu kitakachotuzuwia kufurahi. Nafikiri , mabao 4-0 katika mchezo huo ni matokeo yanayostahili."
Kwa upande wake Borussia Dortmund ambayo katika michezo minne ya Bundesliga msimu huu mlango wake haujatikiswa , jana Jumapili ilionesha kwamba inamedhamiria msimu huu kuipa changamoto Bayern Munich ambayo ni mabingwa watetezi na wanaowania kunyakua taji hilo kwa mara ya sita mfululizo. Borussia Dortmund inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa suluhu kwa pointi na Hannover 96 , lakini ikiongoza kwa mabao.
Lakini ushindi wa mabao 5-0 wa Borussia Dortmund dhidi ya FC Kolon , umeingia doa pale Kolon walipolalamikia bao la pili la Dortmund kutokana na refa kupiga firimbi kabla mpira haujavuka msitari. Mwamuzi aliashiria kwamba mchezaji wa Borussia Dortmund alimsukuma mlinda mlango wa Kolon na hivyo mpira kumponyoka na ukasindikizwa wavuni na mlinzi wa Dortmund Socratis. Refa msaidizi wa video alimfahamisha mwamuzi kwamba wachezaji wa Dortmund hawakumgusa mlinda mlango Timo Horn na kwamba hilo ni bao safi.
Bao hilo linalalamikiwa na viongozi wa FC Kolon kwamba aliwazuwia wachezaji wa Kolon kuzuwia mpira huo kuingia wavuni. Lakini hata hivyo inaonekana dhahiri kwamba katika wakati mpira huo unaelekea wavuni hakuna mchezaji wa Kolon aliyekuwa karibu kuuondoa.
Tukio la kusikitisha lilitokea katika mchezo kati ya Stuttgart na Wolfsburg, ambapo mchezaji wa kati wa Stuttgart Christian Gentner aligongana na mlinda mlango wa VFL Wolfsburg , na Gentner kukutana na goti la mlinda mlago huyo moja kwa moja usoni na kupoteza fahamu na watoa huduma ya kwanza walilazimika kushikilia ulimi wake ili kunusuru maisha yake. Lakini madaktari wanasema hali yake inaendelea vizuri hadi sasa. Mchezo huo ulimalizika kwa Wolfsburg kukubali kipigo cha bao 1-0. Kocha wa Wolfsburg Andries Jonker ambaye nae baada ya matokeo mabaya ya timu hiyo amefutwa kazi hii leo, amesema baada ya pambano hilo kuwa tukio hilo halikuleta sura nzuri katika mchezo huo.
"Kwa kweli huo ni wakati wa kutisha , wakati mlinda mlango akitoka kuufuata mpira, na unafahamu , kwamba wakati wowote kitu chochote kinaweza kutokea, kwamba kunaweza kutokea mgongano. Lakini unamatumaini kila mara , kwamba hakuna mchezaji atakayeumia , bila shaka hakuna mlinda mlango ama mchezaji wa ndani. Hali hiyo si nzuri."
Hannover 96 inayoshika nafasi ya pili baada ya Borussia Dortmund katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga imeendeleza ushindi siku ya Jumamosi baada ya kuikandika Hamburg SV kwa mabao 2-0 siku ya Ijumaa , ambapo ilishika nafasi ya uongozi japokuwa kwa muda tu kwa mara ya kwanza tangu Neil Amstrong wa Marekani kutua mwezini miaka 48 iliyopita.
FC Schalke 04 iliibwaga Bremen kwa mabao 2-1 na kocha wao kijana Domenico Tedesco amesema mchezo huo hata kama ungemalizika kwa sare asingelalamika.
"Kwa ukweli, mchezo huo ungemalizika kwa sare ya mabao 2-2. Lakini tumefurahi na tumeridhika kwa kunyakua pointi zote tatu na tunawatakia Bremen bila shaka katika mchezo ujao kila la kheri."
RB Leipzig yatunisha misuli
RB Leipzig baada ya kuonesha misuli yake wiki iliyopita dhidi ya Freiburg , ilishikwa shati pale ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Boruusia Moenchengladbach. Wakati Bayer Leverkusen chini ya kocha wao mpya Heiko Herlisch ilipata ushindi wake wa kwanza msimu huu baada ya kuirarua Freiburg kwa mabao 4-0.
Hoffenheim ikatoka sare ya bao 1-1 na Hertha BSC Berlin.
Kocha Andries Jonker amekuwa kocha wa kwanza katika Bundesliga kibarua kuota nyasi msimu huu, baada ya Wolfsburg kuamua kutengana nae leo baada ya kupata pointi nne tu katika michezo minne ya Bundesliga.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 raia wa Uholanzi alichukua hatamu za kuiongoza klabu hiyo Februari mwaka huu, baada ya kuacha kazi ya mkufunzi mkuu wa kituo cha vijana wa klabu ya Arsenal London na kufanikiwa kuibakisha Wolfsburg katika ligi ya Ujerumani Bundesliga msimu uliopita, lakini kipigo cha bao 1-0 siku ya Jumamosi dhidi ya VFB Stuttgart kilikuwa ni uthibitisho wa mwisho kwamba ndoa hiyo haiwezi tena kuendelea.
Jonker afutwakazi
Jonker hata hivyo si peke yake , kwani katika Premier League nchini Uingereza, kwani kocha wa Club Anderlecht ya Ubelgiji Rene Weiler amepoteza kazi baada ya klabu hiyo kuanza kwa kusuasua msimu huu. Kufukuzwa kazi kwa Weiler kulitangazwa siku mbili baada ya mashabiki wa klabu hiyo kuandamana nje ya uwanja wakitaka kocha huyo aondolewe kufuatia kikosi chake kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya timu ya chini ya Kortrijk siku ya Jumamosi. Rene Weiler alishinda mataji 34 na klabu hiyo , na kufikia robo fainali ya ligi ya Ulaya , kufuzu kuingia katika awamu ya makundi ya Champions League na kuwatoa vijana wengi kutoka akademi ya klabu hiyo kama Youri Tielemans na Leander Dendoncker, klabu hiyo imesema katika taarifa.
Ligi yarejea tena viwanjani
Timu inayoongoza ligi ya Ujerumani Bundesliga Borussia Dortmund na mabingwa watetezi Bayern Munich wanarejea viwanjani tena katikati ya wiki kuweza kuweka msukumo zaidi katika ushindi wao wa mwishoni mwa juma. Borussia Dortmund inasafiri kwenda kupambana na Hamburg SV siku ya Jumatano , masaa 24 baada ya Bayern kukumbana na Schalke 04 kesho Jumanne.
Kwa upande mwingine wa msimamo wa ligi FC Kolon, Werder Bremen na Freiburg zitahitaji kupata ushindi wao wa kwanza. FC Kolon inapambana na Eintracht Frankfurt , wakati Borussia Moenchengladbach ina miadi na Stuttgart. Augsburg inataka kuendeleza uwezo wake wa kushinda msimu huu itakapopambana na RB Leipzig na Wolfsburg ambayo itafunzwa hivi sasa na kocha Martin Schmidt itajaribu bahati yake dhidi ya Bremen. Hertha inakutana na Leverkusen siku ya Jumatano na Mainz inaikaribisha Hoffenheim siku ya Jumatano.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf , Saumu