1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borrell: Sera za Taliban zinakwamisha msaada kwa Afghanistan

Daniel Gakuba
4 Oktoba 2021

Mkuu wa diplomasia wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mienendo ya Taliban nchini Afghanistan sio ya kuridhisha, na kuonya kuwa hilo linakwamisha juhudi za msaada wa kuepusha kusambaratika kwa uchumi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/41EFf
Frankreich Straßburg | Europäisches Parlament | Josep Borrell
Josep Borrell, Kamishna wa masuala ya nje wa Umoja wa UlayaPicha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance

Hayo Borrell ameyasema akiwa ziarani Saudi Arabia, ambako pia Iran imekuwa kwenye ajenda ya mazungumzo. Kamishna huyo wa masuala ya nje katika Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amewasili nchini Saudi Arabia baada ya kuzizuru pia Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, akizieleza nchi hizo kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika kufufua mkataba baina ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Soma zaidi: Wito watolewa kwa EU kuongeza msaada nchini Afghanistan

Agenda nyingine muhimu katika ziara hiyo ya Borrell ni hali inayojiri nchini Afghanistan chini ya uongozi wa Taliban. Katika mkutano wa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan al Saud, Borrell amesema mienendo ya Taliban

''Bila shaka ni hali ya mtanziko, kwa sababu ikiwa unataka kusaidia uchumi wa nchi usiporomoke, unafikiria kuisadia serikali ya nchi hiyo. Hilo haliwezekani kwa sababu hatutaki kuisaidia serikali hii kutokana na mitazamo wa Taliban, ambayo hadi leo hairidhishi,''  amesema Borrell.

Saudi-Arabien l  Friedensinitiative für Jemen, Außenminister Faisal vin Farhan Al Saud
Faisal bin Farhan al Saud, waziri wa mambo ya nje wa Saudi ArabiaPicha: Saudi Press Agency/dpa/picture alliance

Msaada wa maendeleo wasitishwa

Tangu Taliban kuchukuwa madaraka Afghanistan, Umoja wa Ulaya umeongeza msaada wa kibinadamu, lakini umesimamisha msaada wa kimaendeleo, kama ilivyofanywa na nchi nyingine wafadhali na pia Benki ya Dunia.

Borrell amesema ni mtanziko kwa sababu uchumi wa Afghanistan ukisambaratika janga la kibinadamu litaongezeka, na mivutano itashamiri na kuwafanya watu wengi zaidi watake kuihama nchi hiyo. Katika sintofahamu hiyo, ameongeza Borrell, kiisho cha ugaidi kutokea Afghanistan kitakuwa kikubwa zaidi, hali itakayoathiri jumuiya nzima ya kimataifa.

Afghanistan Kabul | Protest von Frauen, Auflösung durch Taliban
Utawala wa Taliban unatuhumiwa kukanyaga haki za binadamu AfghanistanPicha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Soma zaidi: Mkuu wa sera ya nje ya Umoja wa Ulaya ziarani Uturuki

Kuhusu ukanda wa ghuba, kamishna huyo wa masuala ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema umoja huo unaunga mkono juhudi za Saudi Arabia za kuufanya uchumi wake kuwa wa kisasa zaidi, na kugusia suala la haki za binadamu ambalo limekuwa likiusumbua Umoja wa Ulaya hususan baada ya mauaji ya mwandishi wa habri mkosoaji wa serikali ya Riyadh, Jamal Khashoggi.

Vita vya Yemen ni janga baya

Mzozo wa Yemen pia umeitia doa haiba ya Saudi Arabia, na Borrell ameutaja kuwa ni janga baya. Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia amesema nchi yake inafanya mashauriano ya kina na Marekani kwa lengo la kuumaliza mzozo huo.

Waziri huyo, Faisal bin Farhan al Saud amearifu pia kuwa mazungumzo yanaendelea baina ya nchi yake na hasimu wake wa kikanda Iran, katika juhudi za kupunguza mivutano baina yao.

 

 rtre, afpe