Boris Johnson afanya kikao na baraza lake la mawaziri
25 Julai 2019Johnson ameahidi kuuondoa mkwamo wa Brexit uliosababisha kujiuzulu kwa waziri mkuu wa hapo awali Theresa May. Baadae Waziri Mkuu huyo mpya atatoa taarifa bungeni kuhusu mipango yake ya kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya, na kama ataiondoa nchi yake bila ya mkataba ifikapo Oktoba 31.
Waziri mkuu huyo mpya ameliambia baraza lake jipya la mawaziri kwamba Uingereza imo katika kipindi nyeti kabisa cha historia ya nchi hiyo. Bwana Johnson kwa mara nyingine amesisitiza azma ya kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya itakapofika tarehe 31 mwezi Oktoba au hata kabla ya hapo.
Hata hivyo Waziri Mkuu huyo anatarajiwa kukabiliwa na maswali magumu atakapolihutubia bunge baadae leo. Mwanasiasa huyo amebakiwa na siku100 ili kuweza kuitimiza ahadi ya kuutekeleza mchakato wa Brexit, baada ya kusema kuwa serikali ya waziri mkuu wa hapo awali ilipoteza muda wa miaka mitatu kutokana na kutojiamini katika suala la Brexit.
Kwa upande wake kiongozi wa Ireland Leo Varadkar amesema wazo kwamba Waziri Mkuu mpya Boris Johnson ataweza kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya juu ya kufikia mkataba mpya wa Brexit, haliakisi hali ya ukweli.
Naye kiongozi wa chama cha Democratic Unionist Party, DUP Arlene Forster amesema matokeo ya kura ya maoni juu ya Brexit yanapaswa kutekelezwa.
Wakati huo huo kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn amemtaka Waziri Mkuu mpya Boris Johson akubali kuitisha uchaguzi utakaompa uhalali wa kuongoza nchi. Lakini bwana Johnson ameashiria kwamba haoni ulazima wa kuitisha uchaguzi kabla ya kuutekeleza mchakato wa Brexit, yaani kuiondoa Uingereza Umoja wa Ulaya.
Katika baraza jipya la mawaziri bwana Johnson amewateua watu aliowahi kufanya nao kazi ikiwa pamoja na Waziri mpya wa mambo ya nje Domic Raab, Waziri wa fedha Sajid Javid, Waziri wa Mambo ya Ndani Priti Patel na mnadhimu wa chama cha Kihafidhina bungeni Jacob Rees-Mog.
Vyanzo:/DPA,AFP,APE/https://p.dw.com/p/3MgOJ