1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bobi Wine ashtakiwa kwa Uhaini

23 Agosti 2018

Mbunge wa Uganda ambaye pia ni mwanamuziki mashuhuri Robert Kyagulanyi maarufu ‘Bobi Wine' ameshtakiwa kwa makosa ya uhaini katika Mahakama moja ya kiraia muda mfupi baada ya kuachiwa kutoka mahakama ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/33d3X
Uganda «Präsident der Ghettos» Bobi Wine wegen Hochverrats angeklagt
Picha: picture alliance/AP Photo/Str.

Hati ya mashtaka imesema Kyagulanyi na wenzake walijaribu kumdhuru Rais Yoweri Museveni wakati wa mkasa uliotokea siku kadhaa zilizopita ambapo msafara wa kiongozi huyo ulishambuliwa kwa mawe.

Hakimu wa mahakama hiyo ya kiraia katika mji wa kaskazini wa Gulu ameamuru  Kyagulanyi aendelee kushikiliwa mahabusu hadi Agosti 30 na atafikishwa tena mahakamani na watuhumiwa wengine 34 walioshtakiwa kwa uhaini wiki iiyopita.

Kyagulanyi alikamatwa tena na kufunguliwa mashataka katika mahakama hiyo muda mfupi baada ya kufutiwa mashtaka kuhusu umiliki silaha kinyume na sheria katika mahakama moja ya kijeshi.

Akiwa mahakamani mawakili wake wamesema Wine hawezi kusimama na kutembea mwenyewe.

Mahakama ya Kijeshi yafuta Madai dhidi yake

Hapo kabla waendesha mashtaka wa jeshi waliondoa madai kuhusu umiliki wa silaha yaliyokuwa yakimkabili Kyagulanyi wakati mbunge huyo alipofikishwa kwenye mahakama ya kijeshi na kuonekana kwa mara ya kwanza tangu alipokamatwa wiki iliyopita.

Uganda Sänger Bobi Wine
Picha: DW/E. Lubega

Shirika la habari la DPA limesema wafuasi wa Bob Wine walishangilia na kumkumbatia kwa furaha baada ya mahakama ya kijeshi kutoa uamuzi wa kuyafuta mashataka dhidi yake.

Hata hivyo muda mfupi baada ya uamuzi huo kutangazwa polisi ilimkamata mara moja mwanasiasa huyo na kumfikisha kwenye mahakama ya hakimu mkaazi ya mji wa Gulu.

Bobi Wine alikamatwa na wabunge wengine wanne wa upinzani na watatu kati yao wanakabiliwa na mashataka ya kufanya uhaini. Awali Mawakili wa wanasiasa hao wa upinzani walisema Wine na wenzake waliteswa wakiwa kizuizini na kwamba Wine alikuwa akisumbuliwa na tatizo la figo kutokana na kipigo.

Kadhalika waliliambia shirika la habari la DPA kuwa Mbunge mwenzake Francis Zaake amelazwa hospitali akiwa hajitambui  na anatumia vifaa vya kumsaidia kupumua.

Akiwa mahakamani siku ya Alhamisi, Wine alikuwa akitumia magongo kumsaidia kutembea na alionekana mnyonge na wakati wote alijiinamia.

Serikali ya Uganda na Shinikizo la Kumwachilia 'Bobi Wine'

Uganda Proteste in Kampala
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Kabuubi

Kushikiliwa kwa Bobi Wine kumezusha hasira nchini Uganda na miongoni mwa wasanii maarufu kote ulimwenguni ambao wamelaani pia taarifa ya kupigwa vibaya akiwa kizuizini madai ambayo serikali ya Uganda imekanusha.

Serikali ya Uganda imekabiliwa na shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi hiyo ya kumwachia huru mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 36 na kwa siku kadhaa sasa vyombo vya usalama nchini humo vimetumia nguvu kukabiliana na maandamano  ya mitaani yaliyotaka kushikiliwa Bobi Wine kufikie mwisho.

Watu kadhaa walikamatwa siku ya Jumatatu wakati wakati fujo zilipozuka katikati ya mji wa Kampala na vyombo vya habari viliwaonesha watu waliovalia sare za kijeshi wakiwapiga raia ikiwemo waandishi habari wawili. Jeshi tangu wakati huo lakini limeomba radhi kuhusiana na matukio hayo.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AP/AFPE/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga