1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken na Lavrov wajadili kubadilishana wafungwa

30 Julai 2022

waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani Antony Blinken amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuhusu pendekezo la kubadilishana wafungwa.

https://p.dw.com/p/4EtnR
Bildkombo Außenminister Blinken und Lawrow
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken (kushoto) na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov.

Kwenye mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine, wanadiplomasia hao wawili walijikita zaidi kuzungumzia suala la kubadilishana wafungwa huku kila upande ukishikilia msimamo wake kuhusu vita nchini Ukraine.

Waziri Blinken ametaka Moscow kukubali pendekezo la Washington la kuwaachia huru wamarekani wawili wanaoshikiliwa nchini Urusi.

Blinken amesema mazungumzo hayo yalikuwa ya "dhati na uwazi" na kwamba ameitaka Kremlin iridhie pendekezo la kuwaachia huru Paul Whelan na Brittney Griner, kama sehemu ya awamu mpya ya kubadilishana wafungwa.

Kwenye awamu hii ya sasa Marekani imependekeza kumwachia huru mlanguzi wa silaha wa Urusi Viktor Bout anayetumikia kifungo cha miaka 25 nchini Marekani.

Huko Ukraine Zelenksyy ashuhudia usafirishaji nafaka

Wakati hayo yakijiri Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameitembelea moja ya bandari kwenye Bahari Nyeusi kushuhudia maandalizi ya usafirishaji shehena ya nafaka iliyokwama kwa miezi mitano kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Urusi.

Akiwa kwenye viunga vya bandari ya Chernomorsk jimboni Odessa rais Zelensky alishuhudia upakiaji wa shehena ya nafaka kwenye meli inayopeperusha bendera ya Uturuki ambao unafanywa kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita mnamo Februari 24.

Videostil Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskyy alipoitembelea bandari huko Bahari Nyeusi.Picha: APTN

Aliwaambia waandishi habari kwamba kipaumbele kinatolewa kwa meli ambazo tayari zilikwishapakia shehena ya ngano na mazao mengine lakini zilshindwa kuondoka baada ya kuzuka kwa vita.

Ziara yake ambayo haikutangazwa ni sehemu ya juhudi za Ukraine za kuonesha utayari wake wa kusafirisha mamilioni ya tani za nafaka ikiwa ni utekelezaji wa mkataba uliofikiwa wiki moja iliyopita kati ya nchi hiyo na Urusi huko Instabul, Uturuki.

Mkataba huo unalenga kuruhusu kusafirishwa kwa shehena muhimu ya nafaka na mazao mengine kwenda masoko ya dunia kunusuru mamilioni ya watu wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Ukraine ni msafirishaji mkubwa duniani wa ngano, shayiri, mahindi na mafuta ya alizeti, na kukosekana kwa bidhaa hizo kumetikisa masoko ya vyakula na kupandisha bei kote duniani.

Zeleskyy amesema jeshi la Ukraine liko tayari kufanikisha usafirishaji salama kwa shehena hizo, akiongeza kwamba, "Ni muhimu kwetu sisi kwamba Ukraine inabakia kuwa tegemeo la usalama wa chakula duniani".

Urusi na Ukraine zalaumiana kuhusika na shambulizi dhidi ya gereza

Ukraine I  Olenivka Gefängnis
Picha: RIA Novosti/SNA/IMAGO

Katika hatua nyingine Urusi na Ukraine zimetupiana lawama kwa kila upande kuutuhumu mwingine kuhusika na mashambulizi dhidi ya jela moja inayowahifadhi wafungwa wa kivita wa Ukraine na kusababisha vifo vya wa watu kadhaa.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema mashambulizi hayo yalifanywa na vikosi vya Ukraine kwa kutumia mifumo ya kisasa ya makombora iliyotolewa na Marekani katika kile Moscow imekitaja kuwa kisa cha "uchokozi" kinacholenga kuwazuia wanajeshi kusalimu amri.

Hata hivyo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky  ameituhumu Urusi kuhusika na mashambulizi hayo anayosema yamewauwa zaidi ya watu 50. Zelensky amesema hizo ni hujuma nyingine za Urusi zinazolenga kuwaua raia wa Ukraine katika vita inayoendelea.

Kufuatia mashambulizi hayo Zelensky ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuitangaza Urusi kuwa taifa linalofadhili ugaidi.