1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Blinken awasili Mashariki ya kati kwa mara ya tano

5 Februari 2024

Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken tayari amewasili nchini Saudi Arabia Jumatatu ikiwa ni awamu nyingine ya juhudi za kutafutia mgogoro wa Gaza ufumbuzi.

https://p.dw.com/p/4c41i
Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akishuka kutoka kwenye ndege alipowasili mjini Riyadh Februari 5, 2024.
Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akishuka kutoka kwenye ndege alipowasili mjini Riyadh Februari 5, 2024.Picha: Mark Schiefelbein/AP/picture alliance

Ziara ya Blinken ni sehemu ya juhudi za kutafuta makubaliano mapya ya usitishaji vita kati ya Israel na Hamas, mnamo wakati mashambulizi makali yakiendelea kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kulingana na mwandishi habari wa shirika la habari la AFP, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alitua mjini Riyadh, ikiwa ni ziara ya tano anayofanya Mashariki ya Kati tangu shambulizi la wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, liliposababisha vita.

Soma pia: Umoja wa Ulaya watahadharisha usitishaji msaada UNRWA

Lengo la Marekani kwenye ziara pana ya Blinken Mashariki ya kati ni kujaribu kusogeza mbele mazungumzo ya kurejesha uhusiano kati ya Saudi Arabia na Israel na vilevile kusogeza mbele mazungumzo kuhusu utawala wa baada ya vita vya Gaza.

Ziara yake imejiri mnamo wakati Marekani inafanya mashambulizi ya kulipiza kisasinchini Syria, Iraq na Yemen dhidi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, kufuatia shambulizi la droni wiki iliyopita ambapo wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa nchini Jordan na wengi walijeruhiwa.

Sehemu ya majengo ambayo yameharibiwa Gaza kufuatia vita vilivyoanza baada ya shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7.
Sehemu ya majengo ambayo yameharibiwa Gaza kufuatia vita vilivyoanza baada ya shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7.Picha: Mohammed Hajjar/AP Photo/picture alliance

Juhudi za upatanishi kuwaachilia mateka wa Israel zaendelea

Blinken anatarajiwa kuzuru Misri, Qatar na Israel, kisha baadaye wiki hii ataendeleza pia juhudi zinazoongozwa na Misri na Qatar kupata makubaliano ya wanamgambo wa Hamas kuwaachilia mateka wa Israel.

Akiwa Saudi Arabia anatarajiwa kukutana na mwanamfalme wa taifa hilo Mohammed bin Salman na vilevile waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ya kifalme Faisal bin Farhan A Saud.

Kabla ya kuanza safari, Blinken alitilia mkazo haja ya dharura ya kushughulikia hali ya kiutu ya Gaza, hasa baada ya mashirika ya kutoa misaada kukariri wasiwasi wao kuhusu hali mbaya ya ukanda huo ambao umezongwa na vita kwa takriban miezi minne sasa.

Wapalestina watumai ziara ya Blinken itaepusha mashambulizi zaidi ya Israel

Israel imetishia kuanzisha mashambulizi mapya ya ardhini katika mji wa Rafah.
Israel imetishia kuanzisha mashambulizi mapya ya ardhini katika mji wa Rafah.Picha: Dylan Martine/REUTERS

Wapalestina ambao wanaishi kwa taharuki kufuatia mashambulizi, na mgogoro wa kiutu wamesema wanataraji ziara ya Blinken hatimaye itachangia kupatikana kwa makubaliano haraka kuepusha mashambulizi mapya ya vikosi vya Israel kwenye ukanda wa Gaza.

Wiki iliyopita, wajumbe wa Qatar na Misri, waliwasilisha rasimu ya makubaliano kwa wanamgambo wa Hamas. Lakini wanamgambo hao hawajatoa jibu lao, ila hapo awali wameelezea masharti yatakayohakikisha vita hivyo vya Gaza ambavyo vimedumu kwa miezi minne vinamalizika.

Soma pia: Hamas yazingatia pendekezo la mapatano lililoridhiwa na Israel

Hayo yakijiri, Israel imeendeleza mashambulizi yake katika baadhi ya maeneo yenye makabiliano makali na imetishia kuanzisha mashambulizi mapya ya ardhini katika mji wa Rafah.

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Kulingana na wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 27, 360 wameuawa na vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza tangu vita hivyo vilipoanza.

Vyanzo: RTRE, AFPE