Blinken alaani uchokozi wa Korea Kaskazini
14 Julai 2023Katika majadiliano yaliyohusisha wanadiplomasia wa zaidi ya mataifa 24 waliokutana Indonesia, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Antony Blinken ametoa wito kwa mataifa yanayounda Jumuiya ya Indo-Pasific kuwa kitu kimoja ili kukomesha matumizi ya silaha za maangamizi pamoja na kurusha makombora.
Ametaka pia kuwepo kwa utulivu katika kanda hiyo na kwamba hakuna changamoto kubwa kwa usalama wa kanda hiyo zaidi ya uchokozi wa kurusha makombora unaofanywa na Korea kaskazini.
Soma zaidi:Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Blinken ahimiza utulivu katika Indo-Pasifiki
Lavrov akasirishwa na ukosoaji
Katika hatua nyingine waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amekasirishwa na ukosoaji dhidi ya uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo ya Jumuiya ya kanda ya , Mkuu wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema Lavrov alimjibu kwa ukali kuwa kila kitu kinachoendelea kinatokana na nadharia za kufikirika za magharibi na kwamba vita vitaendelea kwani Urusi haiko tayari kuachana na vita na kuondoa majeshi yake Ukraine.
Tukisalia katika mkutano huo, waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Retno Marsudi amesema kuwa, mkutano wa mataifa ya kusini mashariki mwa Asia umekubaliana kuimarisha diplomasia ya kujilinda. Marsudi ametambua pia ongezeko la mivutano inayoendelea kuigawanya kanda hiyo na kwamba changamoto hiyo inazidi kuwa kubwa. Ukanda huo unapambana kuutatua mzozo wa Myanmar ambayo utawala wake unashutumiwa vikali kwa ukatili dhidi ya raia.