Blinken akutana na mkuu wa Jumuiya ya NATO
13 Novemba 2024Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte, mjini Brussels wakati ambapo utawala unaoondoka wa Rais Biden unataka kuhakikisha juu ya misaada kwa Ukraine kabla ya Donald Trump kurejea madarakani.
Rais mteule Trump, ameutilia mashaka msaada huo kwa Ukraine na anasema atavimaliza vita vya Urusi na Ukraine haraka.
Washirika wa NATO wanahofia huenda Trump akajaribu kuilazimisha Ukraine kukubali amani kwa masharti ya Urusi.
Blinken anatarajiwa kujadiliana mjini Brussels jinsi washirika wa Marekani watakavyoweza kuchukua uongozi juu ya misaada kwa ajili ya Ukraine.
Baadaye Blinken anatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Andrii Sybiha, na pia atakutana na kamanda mkuu wa NATO kanda ya Ulaya Jenerali Christopher Cavoli, viongozi wa Umoja wa Ulaya na waziri mwenzake wa Uingereza David Lammy.