Juhudi za kutatua mzozo wa Hamas na Israel zaendelea Misri
20 Machi 2024Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mathew Miller, amesema Blinken atakutana na viongozi wa Saudi Arabia na Misri mjini Jeddah na Cairo kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Misri pamoja na Qatar kutafuta makubaliano pamoja na kutafuta mbinu za kupeleka misaada zaidi mjini Gaza
Mazungumzo juu ya kusitisha mapigano yameanza tena nchini Qatar, ambaye ni mpatanishi katika majadiliano ya kusitishwa vita kati ya Israel na Hamas, lakini wiki kadhaa za majadiliano makali hayajafanikiwa kufikiwa makubaliano hayo ambayo Marekani inatumai yatasaidia kupunguza mgogoro wa kibinaadamu unaohofiwa kutanuka mjini Gaza.
"Tumekuwa tukifanya kazi kubwa tangu Januari na washirika wetu wa kiarabu na tutaendelea na majadiliano hayo na pia kujadili juu ya suluhu ya muda mrefu ya amani ya kudumu ya Mashariki ya kati. Kazi nyingi zimekuwa zikiendelea kwa wiki na miezi kadhaa iliyopita. na hicho ndicho tutakachoendelea kukifanya huko," alisema Blinken.
Netanyahu aidhinisha operesheni ya Rafah wakati wajumbe wakielekea Doha
Matamshi haya yanakuja wakati kukiwa na mvutano kati ya serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambaye hapo jana alitupilia mbali wito wa Biden aliyetaka Israel iachane na operesheni yake ya ardhini katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza, kunakohifadhiwa mamilioni ya wapalestina waliopoteza makaazi yao kutokana na vita hivyo vilivyoanza Oktoba 7.
Licha ya hayo kuarifiwa waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant anatarajiwa kuizuru Washington wiki ijayo wakati kukiwa na shinikizo hilo la kuachana na operesheni ya mjini Rafah.
Uingereza yasema ni lazima Hamas watokomezwe
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron amesisitiza kwamba ni muhimu kuwe na makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, ili kutoa nafasi ya kuachiwa kwa mateka, lakini akasema bado kuna matakwa mengi yanayopaswa kutimizwa kabla ya kuwa na makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano. Cameron amesema ni lazima viongozi wa Hamas waondolewe mjini Gaza na ni lazima pia kuusambaratisha kabisa mfumo aliouita wa kigaidi mjini humo.
Marekani: Israel imruhusu Mkuu wa UNRWA kuingia Gaza
Huku hayo yakiarifiwa wanajeshi wa Israel wameivamia hospitali ya Al shifa na kuwauwa takriban watu 90 waliokuwa wamejihami kwa silaha na kuwakamata wengine 160. Katika taarifa ya jeshi la Israel wanajeshi hao waliwauwa wale iliyowaita wamagaidi na kupata pia silaha katika sehemu kadhaa za hospitali hiyo kubwa mjini Gaza.
Imesema imetekeleza uvamizi huo kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka mauaji ya raia, wagonjwa na wafanyakazi wa hospitali hiyo pamoja na vifaa vyake. Jeshi hilo limesema limefanya uvamizi huo baada ya taarifa za kijasusi kugundua kuwa hospitali hiyo ya Al Shifaa inatumiwa na watu waliojihami kwa silaha.
Canada nayo imesema itasimamisha usafirishaji wake wa silaha kwa Israel kufuatia hali halisi ya mapigano inayoshuhudiwa kwa sasa.
reuters/afp
Kwa taarifa nyingine za habari, tazama chaneli yetu ya habari.