Blatter: ulimwengu wa kandanda uiheshimu Afrika
3 Aprili 2015Blatter ameyasema hayo kabla ya mkutano mkuu wa Shirikisho la Kandanda Afrika – CAF utakaoandaliwa wiki ijayo. Wapinzani wake katika wadhifa wa urais, ambao wanasema sifa ya FIFA iliyoharibiwa na kashfa nyingi inastahili mageuzi, pia watakuwa katika mkutano huo na wamekuwa wakitafuta uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa Afrika.
Blatter mwenye umri wa miaka 79 anasema“ustadi wa kuburudisha na ubora wa kiufundi wa tmu za Afrika ni miongoni mwa vivutio vikuu katika Kombe la Dunia“. Timu mbili za bara Afrika zilifika katika hatua ya 16 za mwisho katika Kombe la Dunia nchini Brazil kwa mara ya kwanza.
Afrika kwa muda mrefu imemuunga mkono Blatter na imeatangaza kuwa itasimama naye katika uchaguzi wa FIFA mnamo Mei 30.
Wapinzani wake watatu wa urais wa FIFA – Prince Ali bin Al Hussein wa Jordan ambaye ni makamu wa rais wa FIFA, mkuu wa shirikisho la kandanda la Uholanzi Michael van Praag na aliyekuwa mchezaji nguli wa Ureno Luis Figo – wote wanatarajiwa kuwa Cairo kwa mkutano huo mkuu wa CAF.
Wanachama wa 54 wa CAF wanalifanya kuwa shirikisho kubwa zaidi katika upigaji kura za FIFA, mbele ya shirikisho la Ulaya – UEFA ambalo linampinga Blatter kuwania muhula mwingine.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu