Blatter, Platini wafikishwa mahakamani Uswisi
8 Juni 2022Maafisa hao wa zamani wa ngazi za juu katika ulimwengu wa soka wanashtakiwa kwa tuhuma za ulaghai wa kupokea kinyume cha sheria fedha kwa kulitumia shirikisho la FIFA.
Platini anatuhimiwa kupokea faranga milioni 2 za Uswisi kwa kazi aliyoifanya kama mshauri wa shirikisho hilo la soka duniani kati ya mwaka 1998 na mwaka 2002 miongoni mwa makosa mengine. Blatter mwenye umri wa miaka 86 alifika mahakamani akiwa na mwanawe wa kike Corinne wakati Platini mwenye umri wa miaka 66 aliingia na timu yake ya wanasheria. Mchakato wa kesi unaendeshwa kwa lugha ya kijerumani, na kutafsiriwa kwa kifaransa.
Waendesha mashataka wa Uswisi wanazungumzia nyaraka zinazoonesha malipo yasiyoeleweka zilizowasilishwa mbele ya FIFA na Platini mwaka 2011 na kuidhinishwa na Blatter. Kesi hii ilianza kuangaziwa mnamo mwaka 2015 na ndiyo iliyokifikisha mwisho kipindi cha uongozi wa Blatter wa shirikisho hilo la soka duniani.
afp, dpa, ap, reuters