Biden: Tutawaondoa raia wote Afghanistan
21 Agosti 2021Kwanza rais Joe Biden ametoa ahadi bila kupepesa macho kwamba ananuwia kuwarejesha nyumbani raia wote wa Marekani walio nchini Afghanistan pamoja na Waafghani waliosaidia juhudi za nchi yake kwenye vita vya karibu miaka 20.
"Tutawarudisha nyumbani" amesema Biden akiwaahidi Wamarekani ambao bado wamekwama nchini Afghanistan siku kadhaa tangu kundi la Taliban lilipochukua udhibiti wa mji mkuu, Kabul, na kumaliza vita vya zaidi ya miongo miwili.
Matamshi ya rais Biden aliyoyatoa akiwa ikulu mjini Washington yananuwia kupunguza hamkani na shakashaka zilizohanikiza wiki nzima baada ya ulimwengu kushuhudia picha na video zenye kuonesha mtafaruku hususani kwenye uwanja wa ndege mjini Kabul.
Ahadi ya Biden pia kuhusu kutowaaacha nyuma maelfu ya Waafghani ikiwemo wakalimani waliovisaidia vikosi vya Marekani katika operesheni zake chungunzima imelenga kuonesha picha kwamba Washington haikwepi jukumu iliyojitwika.
Matamshi yenye faraja katikati ya kizungumkuti
Hata hivyo matamshi hayo ya kutia moyo kutoka kwa rais Biden yametolewa wakati maelfu ya watu wengi wakiwa Wamerekani na raia wa Afghanistan wanaotaka kuikimbia nchi hiyo wamekwama kwenye uwanja wa ndege mjini Kabul.
Hapo jana iliilazimu Marekani kutuma helikopta zake za jeshi kwenda maeneo yanayodhibitiwa na Taliban kuwabeba raia walioshindwa kabisa kulifikia eneo la Uwanja wa Ndege kunakoendeshwa operesheni ya kuwaondoa nchini Afghanistan.
Utawala wa Biden unaandamwa na ukosoaji mkubwa baada ya mikanda ya video na ripoti kuelezea hali ya mshikemshike na vurugu kwenye viunga vya uwanja wa ndege mjini Kabul.
Duru za ulinzi zinasema hadi sasa ni watu 5,700 pekee ikiwemo Wamarekani 250 ndiyo wameondoshwa nchini Afghanistan na kupelekwa kwenye vituo vya muda vilivyoandaliwa kwenye mataifa jirani.
NATO yajipiga kifua kwa ahadi ya kuratibu kuondolewa kwa raia wa mataifa wanachama
Wakati huo huo mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami NATO jana Ijumaa yamesisitiza nia yao ya kuhakikisha inawaondoa salama raia wake nchini Afghanistan na Waafghani walio kwenye kitisho cha kulengwa na kundi la Taliban.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Jumuiya ya NATO wamekubaliana kufanya kazi pamoja katika kurahisisha utaratibu wa kuwapeleka watu eneo la uwanja wa ndege, kuwapatia nyaraka zinazohitajika kwa wakati na kuwasafirisha kutoka Afghanistan haraka iwezekanavyo.
Majadiliano ya viongozi hao wa NATO yamefanyika katika wakati ripoti zinasema ndege za mataifa ya jumuiya hiyo zimelazimika kuondoka tupu kwa sababu ya kujikongoja kwa utaratibu wa kushughulikia vibali na nyaraka nyingine
Katika hatua nyingine waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema hadi sasa mataifa 13 yamekubali kuwapokea na kuwahifadhi kwa muda raia wa Afghanistan waliohamishwa na Marekani kukimbia hujuma kutoka kundi la Taliban.
Blinken amesema wakimbizi hao wa Afghanistan watapewa hifadhi kwenye mataifa ya Albania, Canada, Colombia, Costa Rica, Chile, Kosovo, North Macedonia, Mexico, Poland, Qatar, Rwanda, Ukraine na Uganda.