1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndonesia

Biden na Xi wakutana mjini Bali nchini Indonesia

14 Novemba 2022

Kiongozi wa China Xi Jinping na Rais wa Marekani Joe Biden, wamekutana kwa mazungumzo wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili uko chini zaidi katika muda wa miongo kadhaa

https://p.dw.com/p/4JVWA
USA Mid Terms Wahlen Demokratie Wähler Wahlurne Joe Biden
Picha: Oliver Contreras - Pool via CNP/picture alliance

Viongozi hao wawili wamekutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza mjini Bali nchini Indonesia tangu Biden kuchaguliwa kuwa rais, siku moja kabla ya mkutano wa mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani na yale yanayoinukia kiviwanda G20 unaotarajiwa kuanza hapo kesho Jumanne unaotazamiwa kugubikwa na mvutano kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Biden amemwaambia Xi kwamba anafurahia kumuona na kuongeza kuwa amejitolea kuweka wazi njia zake za mawasiliano katika viwango vya kibinafsi na kiserikali.

Biden asema China na Marekani zapaswa kuonesha zinaweza kudhibiti tofauti zao

Biden ameongeza kuwa Kama viongozi wa mataifa hayo mawili, wanawajibu wa kuonyesha kwamba China na Marekani zinaweza kudhibiti tofauti zao, kuzuia ushindani kuwa kitu chochote karibu na migogoro, na kutafuta njia za kufanya kazi pamoja katika masuala ya dharura ya kimataifa yanayohitaji ushirikiano wao wa pamoja. Biden pia alitaja mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa chakula cha kutosha kuwa matatizo ambayo dunia inatarajia mataifa hayo mawili kushughulikia.

Biden na Xi wakubaliana kwamba silaha za nyuklia hazipaswi kutumika

China Peking | Parteitag der Kommunistischen Partei
Rais wa China - Xi JinpingPicha: Andy Wong/AP Photo/picture alliance

Baada ya mazungumzo hayo yaliochukuwa takriban masaa matatu, Ikulu ya Marekani ya White House, imesema kuwa wakati wa mazungumzo hayo, viongozi hao wawili pia wamekubaliana kwamba silaha za nyuklia hazipaswi kutumika ikiwa ni pamoja na nchini Ukraine. Ikulu hiyo imeongeza kuwa Biden aliibua pingamizi dhidi ya kile alichokiita vitendo vya kulazimisha na vya uchokozi vya China dhidi ya Taiwan na kumuambia Xi kwamba dunia inapaswa kuishinikiza Korea Kaskazini kuchukuwa hatua za kuwajibika baada ya rekodi ya msururu wa urushaji wa makombora na hofu inayoongezeka ya majaribio ya nyuklia.

Xi asema uhusiano wa China na Marekani haukidhi matarajio ya kimataifa

Akimjibu Biden, Xi amesema kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili haukidhi matarajio ya kimataifa. Xi ameongeza kusema kuwa wanahitaji kupanga utaratibu sahihi kwa uhusiano kati ya China na Marekani na kwamba pia wanahitaji kutafuta njia ya sawa ya uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kuelekea mbele na kuuimarisha zaidi. Xi amesema dunia inatarajia kwamba China na Marekani zitashughulikia vyema uhusiano huo na kuongeza kuwa anatazamia kushirikiana na Biden kurejesha uhusiano huo katika utaratibu wa sawa.

Kulingana na shirika la habari la serikali ya China CCTV, Xi amesema hali ya sasa ya uhusiano kati ya China na Marekani haiko katika maslahi ya mataifa hayo mawili na kwamba wanahitaji kuongoza katika mkondo huo. Xi pia amesema wanapaswa kufikiri kuhusu kufafanua mwelekeo wa maendeleo ya nchi zao wenyewe, pamoja na  kuzingatia njia ya kupatana na mataifa mengine.