Biden na Trump washinda chaguzi za awali Michigan
28 Februari 2024Rais Joe Biden ameshinda kirahisi uchaguzi wa awali wa chama chake cha Democratic katika jimbo la Michigan lakini kura ya upinzani iliyopigwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho wenye ghadhabu kutokaka na hatua ya Biden kuunga mkono vita vya Israel dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza umewashangaza waandaaji wa uchaguzi huo na kuvuka mipaka ya matarajio yao.
Katika jimbo la Michigan ambako ni nyumbani kwa idadi kubwa ya Wamarekani wenye asili ya kiarabu, wapiga kura wa chama cha Democratic walihimizwa waandike katika kura zao kwamba hawajaamua kujitolea kumuunga mkono Biden katika hatua ya kupinga sera ya Biden kuhusu vita vya Gaza. Haikufahamika ni kur angapi ziliuzoandikwa maneno hayo.
Wamarekani wengi wa asili ya kiarabu Michigan waliomuunga mkono Biden mwaka 2020, wameghadhabishwa na hatua ya Biden kuunga mkono harakati ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na Hamas, ambako maalfu ya Wapalestina wameuliwa.
Soma pia: Trump na Biden wawania kura za vijana
Muwakilishi wa jimbo la Michigan wa chama cha Democratic Abraham Aiyash amesema, "Kwa hiyo msijaribu kubadilisha maelezo baada ya usiku wa leo kwamba chama cha Democratic kinapasuka. Tunajaribu kukiokoa chama cha Democratic kutokana na mauaji ya halaiki. Tunajaribu kukiokoa chama cha Democratic kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu na kutojali ubinadamu wa ndugu na dada zetu Wapalestina."
Waandaaji wa kampeni wameapa kuwasilisha ajenda yao ya kupinga vita kwenye mkutano mkuu wa chama utakaofanyika huko Chicago mwezi Agosti.
Kampeni ya Trump yapania kushinda uteuzi katikati ya Machi
Kwa upande mwingine, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump naye ameshinda uchaguzi wa awali wa chama cha Republican kwa kura nyingi, huko Michigan na kuimarisha nafasi yake ya kushinda uteuzi wa chama huku akimuacha mbali katika nafasi ya pili mpinzani wake wa mwisho aliyebaki, Nikki Haley.
Trump alisema, "Novemba hii, jimbo la Michigan litamwambia Joe Biden mpotovu, umetimuliwa, toka madarakani. Rais mbaya kabisa kuwahi kuwa naye."
Trump sasa ameshinda katika majimbo yote matano ya kwanza katika kalenda ya uchaguzi wa awali wa chama cha Republican. Ushindi wa Trump dhidi ya mpinzani wake mkubwa, Nikki Haley, unakuja baada ya rais huyo wa zamani kumshinda kwa asilimia 20 katika jimbo lake la nyumbani la South Carolina Jumamosi iliyopita.
Timu ya kampeni ya Trump inapania kupata kura za wajumbe 1,215 zinazohitajika kushinda uteuzi wa chama cha Republican kufikia katikati ya mwezi Machi.
Ingawa Biden na Trump walitarajiwa kushinda kirahisi katika chaguzi zao tofauti, matokeo ya kura zote yanafuatiliwa kwa karibu kuona dalili za uungwaji mkono.
(rtre, aptn)