Biden na Merkel wakutana mjini Washington
16 Julai 2021Viongozi hao wawili yaani Kansela Angela Merkel na mwenyeji wake rais Joe Biden wameahidi kwa uwazi nia yao ya kuendelesha ushirikiano kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya katika ziara ambayo yumkini itakuwa ya mwisho kwa Merkel mjini Washington.
Merkel ambaye amekuwa kiongozi wa kwanza wa serikali kutoka Ulaya kukaribishwa ikulu ya White House na rais Joe Biden tangu alipoapishwa mwezi Januari, amefanya ziara hiyo akinuwia kuimarisha tena mahusiano kati ya Berlin na Washington yaliyopwaya enzi ya rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.
"Sisi siyo tu washirika bali pia ni mataifa yenye urafiki wa karibu" amesema Kansela Merkel baada ya mazungumzo marefu na rais Biden.
Biden amemshukuru Kansela Merkel kwa uongozi wake na kusema wakati anajitayarisha kuwachia wadhifa huo baada ya miaka 16 ya kuiongoza Ujerumani, mahusiano kati ya nchi hizo mbili yataendelea kuwa imara chini ya misingi aliyoijenga.
Viongozi hao wawili kwa pamoja wameahidi nia yao ya kushirikiana kwa karibu kuhimiza amani, usalama na ustawi kote duniani.
Tofauti kuhusu mradi wa Bomba la Gesi bado ni kubwa
Lakini pia wamewaka wazi kwamba wanatofautiana pakubwa kuhusu suala la mradi wa bomba la kusafirisha gesi la Nord Stream 2 litakalosambaza gesi ya Urusi barani Ulaya kupitia Ujerumani.
"Hata marafiki wa karibu huwa na mitazamo tofauti" amesema Biden na kuongeza kwamba kwa mara nyingine amemweleza Kansela Merkel wasiwasi wake kuhusu mradi huo.
Mradi huo wa dola bilioni 11 umekuwa kitovu cha msuguano kati ya Marekani na Ujerumani, huku Washington ikisema unaleta kitisho cha usalama kwa kuongeza utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya gesi kutoka Urusi.
Mataifa mengine pia wanachama wa Jumuiya ya Kujihami NATO wanaupinga mradi huo wa bomba la gesi.
Hata hivyo Merkel amemhakikishia rais Biden kuwa kwa Ujerumani mradi huo ni wa nyongeza tu na haubadili msimamo wake ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya magharibi na mataifa rafiki mfano wa Ukraine.
Merkel atunukiwa shahada ya uzamivu
Kabla ya kukutana na rais Biden, kansela Merkel alifanya mazungumzo na makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris, viongozi wa sekta ya biashara nchini Marekani na pia kuhudhuria hafla ya kutunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu na chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Katika hotuba yake chuoni hapo Kansela Merkel alitoa wito wa kufanyika majadiliano zaidi ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kupewa nguvu ya kutosha kutafuta majibu ya changamoto za ulimwengu.
Kansela Merkel amefanya ziara 20 nchini Marekani katika muhula wake wa miaka 16 na amekutana na marais wanne wa taifa hilo tangu alipoingia madarakani mnamo 2005.
Alikuwa na mahusiano mazuri na marais George Bush na Barack Obama lakini mahusiano yake na Donald Trump yaliingia doa baada ya Trump kumshambulia kutokana na sera yake ya kuruhusu idadi kubwa ya wahamiaji nchini Ujerumani.