1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kukutana na waziri mkuu wa Sweden mjini Washington

5 Julai 2023

Rais Joe Biden wa Marekani atamkaribisha waziri mkuu wa Sweden Ulf Kristersson kwa mkutano unaolenga kuonesha mshikamano na taifa hilo la Scandinavia kuhusu dhamira yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

https://p.dw.com/p/4TRXd
Ulf Kristersson Sweden
waziri mkuu wa Sweden Ulf Kristersson Picha: Ninni Andersson/Government Offices of Sweden/Xinhua/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani leo atamkaribisha ikulu mjini Washington waziri mkuu wa Sweden Ulf Kristersson  kwa mkutano unaolenga kuonesha mshikamano na taifa hilo la Scandinavia kuhusu dhamira yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Soma pia: NATO yasema wakati ni sasa wa kuruidhia maombi ya Finland na Sweden kujiunga na jumuiya hiyo

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya White House imesema Biden na Kristersson watatathmini ushirikiano wa usalama baina ya mataifa hayo mawili na kusisitiza mtazamo wao kuwa Sweden inafaa kujiunga na NATO haraka iwezekanavyo.

Jumuiya ya NATO ilikuwa na matumaini kuwa uanachama wa Sweden utaidhinishwa kabla ya mkutano wa kilele utakaofanyika nchini Lithuania baadaye mwezi huu lakini mipango hiyo imetiwa kiwingu na Uturuki inayokataa kuridhia maombi ya taifa hilo.

Utawala wa rais Reccip Tayyip Erdogan unaituhumu serikali mjini Stockholm kwa kuchukua msimamo laini dhidi ya makundi yanayotishia usalama wa Uturuki hususani taasisi za jamii ya Wakurdi.