Biden aweka malengo makubwa ya chanjo kwa Wamarekani
12 Machi 2021Rais Biden ameyasema hayo katika hotuba ambayo imetolewa sambamba na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu shirika la afya ulimwenguni - WHO kuvitangaza virusi vya corona kuwa janga ya kidunia
''Kwanza, usiku wa leo natangaza kuwa nitayaelekeza majimbo yote, makundi ya kikabila na maeneo yaliyo chini ya himaya ya Marekani, kuhakikisha kuwa watu wote wenye umri wa miaka 18 na zaidi, watakuwa na haki ya kupata chanjo kabla ya Mei mosi.'' Amesema Biden.
Soma Zaidi: Vifo vya Covid-19 vyapindukia 500,000 Marekani
Kiongozi huyo ameanisha pia hatua nyingine za kupamba na ugonjwa huo ambao tayari umeangamiza maisha ya Wamarekani zaidi ya 530,000.
Mshikamano katika majonzi na matumaini
Rais huyo amesema mnamo mwaka mmoja uliopita, Wamarekani wameungana katika maumivu na majonzi, na kuongeza kuwa vile vile wanaunganishwa na matumaini mema ya siku za usoni.
Ametabiri juu ya uwezekano wa Wamarekani kuweza kujumuika tena katika makundi madogo madogo wakati wa sherehe za uhuru wa nchi yao zinazofanyika tarehe nne Julai; lakini ikiwa kabla ya hapo wataendelea kuheshimu maelekezo ya wataalamu wa afya.
Biden ameitoa hotuba yake hiyo baada ya kusaini sheria ya mpango wa afueni wenye thamani ya dola trilioni 1.9, ambao amesema utasaidia kuvishinda virusi vya corona, kuufufua uchumi na kuwapa Wamarekani wenye mahitaji msaada wa moja kwa moja wa kifedha.
Soma zaidi: Biden azindua mpango wa uokozi wa dola trilioni 1.9
Chini ya mpango huo, Wamarekani wengi watapata hundi ya dola 1,400 mara moja, na dola 300 za msaada wa kila wiki kwa wale wasio na ajira, hadi mwezi Septemba.
Chanjo ya AstraZeneca yatiliwa shaka, yasimamishwa na baadhi ya nchi
Kwingineko, Mataifa kadhaa ya Ulaya yamesimamisha kutumia chanjo ya COVID-19 ya AstraZeneca, baada ya ripoti kuwa chanjo hiyo ilisababisha kuganda kwa damu miongoni mwa baadhi ya watu walioipokea. Denmark, Iceland na Norway ni miongoni mwa nchi hizo zilizochukua hatua hiyo ya tahadhari.
Hata hivyo, mataifa hayo yalijizuia kusema moja kwa moja kuwa chanjo hiyo ndio sababu ya tatizo hilo la kuganda kwa damu.
Denmark imesema itasitisha utoaji wa chanjo ya AstraZeneca kwa siku 14, na waziri wake wa afya Magnus Heunicke amesema kwa wakati huu hawawezi kusema kwa uhakika kuwa chanjo hiyo ina uhusiano na tatizo hilo la damu.
Mtaalamu wa tiba ya maradhi yanayosababishwa na virusi kutoka taasisi ya magonjwa ya kitropiki iliyoko mjini London, Polly Roy, ameiambia DW kuwa huwenda tatizo hilo halina uhusiano na chanjo yenyewe, bali matatizo waliyokuwa nao wagonjwa walioathirika.
ape, afpe