Biden awarai Warepublican kufanya kazi naye
8 Februari 2023Hiyo ndiyo ilikuwa hotuba ya kwanza ya Biden kwa Baraza la Wawakilishi tangu Warepublican walipochukua udhibiti wa baraza hilo kwenye uchaguzi wa Novemba mwaka uliopita.
Biden alijaribu kulihakikishia taifa lake kwamba chini ya uongozi wake, nchi imepata mafanikio ya ndani na hata nje huku akidhamiria kuthibitisha kufaa kwake kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao.
Rais Biden atoa rai kupitishwa mageuzi ya idara za polisi
Amesifu ukuaji wa uchumi ambao umeunda nafasi za ajira milioni 12, na juhudi zilizofanikisha kulishinda janga la Uviko-19.
Biden pia amesema demokrasia imeimarika tena nchini Marekani baada ya mitikisiko mwishoni mwa utawala wa mtangulizi wake, ambayo ameitaja kuwa kitisho kikubwa zaidi kwa demokrasia ya Marekani tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wito wa kuepukana na mikwaruzano ya kisiasa
Pia aliangazia maeneo ya mafanikio ya pande mbili katika miaka miwili ambayo amekuwa madarakani, ikiwemo miundombinu muhimu ya majimbo na utengenezaji wa teknolojia wa hali ya juu.
Alisisitiza kuwa Wamarekani wamewapa ujumbe wa wazi kwamba hawataki mivutano kwa sababu ya uchu wa madaraka, na kwamba mikwaruzano isiyo na sababu haitawapeleka popote. Na ndilo lengo lake, kuujenga upya uti wa mgongo wa Marekani, na kuunganisha nchi ili kumaliza kazi.
"Unajua marafiki zangu Warepblican, kama tuliweza kufanya kazi pamoja katika Bunge lililopita, hakuna sababu ya kutoweza kufanya kazi pamoja na kupata makubaliano kuhusu mambo muhimu katika bunge hili pia.”
Kiongozi huyo wa Marekani ameahidi mageuzi katika sekta kadhaa, ikiwemo ya tiba na uendeshaji wa jeshi la polisi.
Changamoto dhidi ya Biden
Lakini changamoto dhidi ya Biden ni nyingi ikiwemo uchumi usiokuwa na uhakika, vita vya Ukraine, kuongezeka kwa mvutano baina ya nchi yake na China na nyinginezo.
Na ishara za kiwewe zisizoepukika kutokana na uvamizi wa bunge Januari 6, 2021, wabunge waliohudhuria wakikabiliana na usalama ulioimarishwa kuliko kawaida.
Kuanzia mwanzo, migawanyiko ya vyama ilikuwa dhahiri bungeni. Wademokrats akiwemo makamu wa rais Kamala Harris walinyanyuka kumpongeza Biden alipoanza hotuba yake. Lakini spika mpya wa bunge ambaye ni Mrepublican Kevin McCarthy, alisalia ameketi kwenye kiti chake.
Badala ya kuzungumzia mapendekezo yake ya sera za kuvutia, Biden aliamua kuangazia tathmini ya hali halisi ya nchi, na akasema kuwa miaka miwili baada ya shambulio la majengo ya bunge, demokrasia ya Amerika haijayumba wala kuvunjika.
Robo moja pekee ya Wamarekani wanahisi mambo yanaenda vyema
Rais Biden alitoa hotuba yake mnamo wakati robo ya watu pekee nchini humo ndio wanasema mambo yanaenda vizuri. Hayo ni kulingana na uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na kituo cha utafiti cha NORC cha shirika la habari la Associated Press
Robo tatu ya watu nchini humo wanahisi mambo yanaenda mrama. Aidha Wademokrat wengi hawataki Biden kuwania muhula mwingine wa urais.
Hotuba ya Biden imejiri siku chache tu tangu alipoliamuru jeshi lake kudungua puto la China lililodaiwa kuwa la kijasusi lililogunduliwa katika anga ya Marekani.
Soma hii pia China yaishtumu Marekani kutumia nguvu baada ya puto lake kudunguliwa.
(Vyanzo: AP, RTRE)