Biden asema mashambulizi ya Israel yanapasa kusitishwa
9 Februari 2024Rais huyo wa Marekani alisema kwamba watu wasio hatia wamekuwa wakipoteza maisha kwenye operesheni hiyo ya Israel.
"Nina mtazamo kama mnavyojua, kwamba uendeshaji wa operesheni ya majibu umepitiliza. Kuna watu wengi wasio na hatia wanaokufa kwa njaa, watu wengi wasio na hatia ambao wako katika shida na kufa. Na haina budi kusimama." Alisema.
Soma zaidi: Blinken aondoka Mashariki ya Kati bila mafanikio
Hatua ya Marekani kuunga mkono vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas imesababisha mkururo wa mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati, pamoja na ukosoaji dhidi ya utawala wa Biden kutoka ndani na nje ya nchi hiyo.
Miezi kadhaa ya mashambulizi na mzingiro wa Israel vimezidisha mzozo wa kiutu kote Gaza.
Lakini Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 alisema ameshinikiza kuruhusu uingizaji wa misaada ya kibinaadamu katika eneo hilo.