Beijing yaanzisha mazoezi katika Bahari ya China Kusini
20 Mei 2022Ofisi ya Usalama wa Baharini katika kisiwa cha kusini cha mkoa wa Hainan imesema mazoezi hayo yalianza Alhamisi na yataendelea hadi Jumatatu.
Aidha, mamlaka hiyo imeendelea kuwa ndege na vyombo vingine vitapigwa marufuku kuingia eneo hilo bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi. Beijing inadai Bahari ya kusini ya China kwa ujumla wake pamoja na njia muhimu ya majini ambayo imekuwa chanzo cha migogoro barani Asia.
Soma zaidi: Biden akutana kwa mara ya kwanza na viongozi ASEAN
Marekani ambayo kwa kawaida huwa haichukui msimamo katika diplomasia yake ya kigeni kuhusu masuala ya uhuru, lakini inasisitiza juu ya haki ya kuendesha shughuli kwa uhuru baharini na mara kwa mara meli zake za kivita zimekuwa zikisogea karibu na visiwa vinavyoshikiliwa na jeshi la China katika eneo hilo kwa kigezo cha kile kinachoitwa "uhuru wa shughuli za kurambaza".
Mara kwa mara China imekuwa ikipinga shughuli kama hizo, ikitaja kuwa ni chokochoko za makusudi zinazohatarisha amani na utulivu.
Ili kutilia mkazo madai yake, China imejenga viwanja vya ndege na miundombinu kadhaa ya kijeshi juu ya visiwa vilivyotengenezwa na binadamu na vilivyojengwa juu ya miamba.
Madai ya nchi zengine
Brunei, Malaysia, Ufilipino na Taiwan pia hutoa madai tofauti katika Bahari ya China Kusini. Tangu mwanzoni mwa mwezi huu, meli inayobeba ndege ya China, inayofahamika kama "Liaoning", imekuwa ikiendesha shughuli zake katika Bahari ya Japani, na Wizara ya Ulinzi imeelezea harakati hizo kama "mafunzo ya kawaida yanayolenga kuboresha utendaji kazi kwa kuzingatia sheria za kimataifa na bila kumlenga yeyote.
Siku ya Jumatano, vyombo vya habari vya China viliripoti kuwa nchi hiyo ilirusha pia ndege za masafa marefu zenye uwezo wa nyuklia za H-6 kupitia eneo hilo.
Soma pia:Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine
Akiwa nchini Japan, Biden atakutana siku ya Jumanne na viongozi wenzake wa chama cha Muungano wa kimkakati wa Indo-Pacific unaojulikana kama Quad, kundi ambalo linajumuisha Australia, India na Japan.
Mataifa hayo manne yana wasiwasi kuhusu ukuaji wa kikanda wa China, uthubutu wake na uwezo unaozidi wa vikosi vya kijeshi.
China inaliona kundi hilo kama sehemu ya msukumo unaoongozwa na Marekani ili kuzuia kushamiri kwake kiuchumi na kisiasa lakini pia kukatisha tamaa juhudi zake za kuishinikiza Taiwan inayojitawala katika kukubali matakwa ya Utawala wa Beijing.
Siku ya Jumatano, wakati akizungumza kwa njia ya kimtandao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Yoshimasa Hayashi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alikosoa kile alichokiita hatua hasi za Washington na Tokyo dhidi ya Beijing.