1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Biden aipa Ukraine idhini kutumia silaha zake dhidi ya Urusi

31 Mei 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ameipa Ukraine idhini ya muda kutumia silaha za Marekani kushambulia ndani ya Urusi kwa lengo la kutetea mji wa Kharkiv. Haya yamearifiwa na maafisa wawili wa Marekani wanaofahamu suala hilo

https://p.dw.com/p/4gTMw
Rais wa Marekani Joe Biden akizungumzia kuhusu vurugu katika chuo kikuu akiwa katika ofisi yake ya Ikulu ya White House mnamo Mei 2, 2024
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Chris Kleponis/ZUMA Wire/Imago Images

Maafisa hao waliozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, wamesisitiza kuwa sera ya Marekani inayoitaka Ukraine kutotumia makombora yake ya masafa marefu pamoja na zana nyingine kushambulia ndani ya Urusi bado haijabadilika.

Soma pia:Mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya washindwa kufikia makubaliano kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za mataifa hayo katika ardhi ya Urusi

Uamuzi huo wa Biden uliripotiwa kwanza na shirika la habari la Marekani, Politico.

Hatua hiyo inakuja wakati maafisa wa Ukraine wameimarisha wito kwa utawala wa Marekani kuruhusu vikosi vyake kujilinda dhidi ya mashambulizi kutoka eneo la Urusi.

Vizuizi vya matumizi ya silaha vyaiweka Ukraine katika hali ngumu

Maafisa wa Ukraine, haswa Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskyy, wamekuwa wakisema kuwa vizuizi vya kutotumia silaha za magharibi dhidi ya Urusi vinaviweka vikosi vya nchi hiyo katika hali ngumu wakati Urusi ikizidisha mashambulizi katika eneo la kaskazini mashariki la Kharkiv.