1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ahadi ya Biden kwa Ukraine: Tutasimana nanyi hadi mwisho

20 Februari 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amefanya ziara ya kustukiza mjini Kyiv Jumatatu, na kumuahidi Rais Volodymyr Zelenskiy kwamba Washington itasimama na Ukraine kadiri itakavyohitajika, kueleka mwaka mmoja wa uvamizi wa Urusi.

https://p.dw.com/p/4Nkdh
Ukraine Krieg l US-Präsident Biden besucht den ukrainischen Präsidenten Selenskyj in Kiew
Picha: Ukrainian Presidential Press Service/via REUTERS

Ziara hiyo ya Ukraine imekuja wakati muhimu katika vita hivi wakati Biden akitazamia kuendeleza umoja wa washirika katika uungaji mkono wao kwa Ukraine katika wakati  vita vikitarajiwa kuongezeka huku pande zote mbili zikijiandaa kwa mashambulizi makali ya ya majira ya machipuko.

Zelenskyy anashinikiza washirika kuharakisha uwasilishaji wa mifumo ya silaha iliyoahidiwa na anayataka mataifa ya Magharibi kutoa ndege za kivita kwa Ukraine - jambo ambalo Biden hadi sasa amelikataa.

Soma pia:Biden asema kuisaidia Ukraine ni jukumu la ulimwengu mzima 

Akiwa Kyiv, Biden ametangaza nyongeza ya dola nusu bilioni katika msaada wa Marekani, ukijumuisha makombora ya vifaru, makombora ya kushambulia vifaru, rada za uchunguzi wa angani na misaada mingine lakini hakuna silaha mpya za kisasa. 

US-Präsident Biden in Kiew
Rais Biden na Zelenskiy wakitemebelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Michael, lililoko katika mji mkuu Kyiv, Februari 23, 2023.Picha: Kay Nietfeld/picture alliance/dpa

Zelenskyy amesema yeye na Biden wamezungumza kuhusu silaha za masafa marefu na nyingine ambazo bado zinaweza kutolewa kwa Ukraine ingawa hazikutolewa hapo awali.

Akizungumza katika mkutano na Biden, Zelenskiy amesema ziara hiyo inatuma ujumbe kwamba jaribio la Urusi kuanzisha mashambulizi mapya halitakuwa na nafasi, huku akimshukuru Biden na Wamarekani kwa msaada usioyumba.

Soma pia:Biden, Zelenskiy wajaribu kuizuwia Congress kusitisha msaada 

Ujumbe wa Biden: Tutasimama nanyi kadiri itakapohitajika

Biden alipata kujionea kwa muda mfupi madhila na hofu wanamoishi Waukraine kwa takribani mwaka mmoja, huku ving'ora vya mashambulizi ya anga vikilia katika mji mkuu wakati yeye na Zelenskiy walipokuwa wakitoka kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Michael, ambalo walitembelea pamoja.

Ujumbe wa Biden katika ziara yake ya Kyiv, aliyoifanya kabla ya safari iliyopangwa ya Warsaw, Poland, ni kusisitiza kwamba Marekani iko tayari kusimama na Ukraine kadiri itakavyohitajika kufurusha vikosi vya Urusi, hata wakati uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha kwamba msaada wa Marekani na washirika katika kutoa silaha na msaada wa moja kwa moja wa kiuchumi umeanza kupungua.

Ukraine Krieg l US-Präsident Biden besucht den ukrainischen Präsidenten Selenskyj in Kiew
Rais Joe Biden akitembea karibu karibu na mwenyeji wake Volodymyr Zelenskiy alipofanya ziara ya kustukiza mjini Kyiv, Februari 20, 2023.Picha: Dimitar Dilkoff/AFP

Baada ya mzungumzo na zelenskiy, Biden aliutemebelea ubalozi wa Marekani mjini Kyiv, kabla ya kuondoka mji mkuu kwa mujibu wa ripoti ya ikulu ya White House.

Anatarajiwa kuwasili nchini Poland kesho Jumanne, ambako atatao hotuba kubwa mjini Warsaw, saa chache kabla ya hotuba kwa taifa ya rais Vladmir Putin mjini Moscow, ambayo inatazamiwa kwa sehemu kubwa kujikita katika mzozo nchini Ukraine.

Chanzo: Mashirika