1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye kubakia korokoroni hadi mwaka ujao

10 Desemba 2024

Mwanasiasa maarufu nchini Uganda na mpinzani mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, Daktari Kizza Besigye, atabaki gerezani hadi mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/4nyOm
Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini UgandaKizza Besigye
Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini UgandaKizza Besigye.Picha: BADRU KATUMBA/AFP

Hii ni baada ya mahakama ya kijeshi kuahirisha leo kusikiliza kwa kesi dhidi yake hadi tarehe 7 Januari 2025. Kundi la mawakili wake lilikuwa limeomba kupewa muda kujadiliana na mwanasiasa huyo na mwenzake, Haji Obeid Lutale, kuhusu maamuzi yao.

Kufuatia hatua ya baraza la kisheria la Uganda kukataa kumpa leseni kiongozi wa mawakili hao Martha Karua, walitaka kushauriana na wateja wao kuwaelekeza jinsi watakavyoendesha kesi hiyo. Ila mahakama iliamua kwamba kundi hilo l mawakili 40 walihitaji muda wa kutosha kufikia maamuzi hayo.

Baraza la kisheria la Uganda lilikataa kumpa leseni wakili na mwanasiasa wa Kenya Martha Karua kwa madai kwamba lengo lake kushiriki katika kesi hiyo halikuwa na  kitaaluma ila la kisiasa. Kwa msingi huo, Martha Karua hangeongoza mawakili wenzake katika kumtetea Dkt Kizza Besigye na mwenzake.

Besigye na Lutale walikamatwa nchini Kenya katika mazingira ya kutatanisha na kisha kusafirishwa kisirisiri kutoka Nairobi hadi Kampala na kufunguliwa mashtaka ya kupatikana na bastola na kuwa na kupanda njama ya kuvuruga usalama wa Uganda.

Kuhusiana na kukamatwa huko, kundi la mawakili limewasilisha malalamiko katika mahakama ya jumuiya  ya Afrika Mashariki wakizitaka serikali za Kenya na Uganda kuwajibikia kwa kile wanachokitaja kuwa utekaji nyara kinyume na sheria na haki za binadamu.