Bernard Membe arejea CCM
29 Mei 2022Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa imemrejeshea kadi ya uanachama aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye serikali ya awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bernard Camilius Membe. Membe amerejea CCM akitokea chama cha ACT-Wazalendo alikohamia na kugombea nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi uliopita.
Zoezi hilo limefanywa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Shaka Hamdu Shaka leo katika kijiji cha Chiponda Rondo,wilaya ya Lindi mkoani Lindi.
Shaka amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya Bernard Membe kuomba msamaha wa kurudishiwa uanachama baada ya kufukuzwa Februari 28, 2020 kutokana na kutuhumiwa kwa makosa ya kimaadili.
Membe ameiambia hadhira iliyojitokeza kushuhudia tukio hilo kuwa amerudi CCM kwa kuwa hakuna tena sababu za kumzuia kutokuwa mwanachama bila kufafanua kwa kina.
Salma Mkalibala