BERLIN: Manazi mamboleo kubanwa zaidi
9 Machi 2005.
Mwakilishi wa jamii ya Kiyahudi nchini Ujerumani amesema anaridhika na mipango ya serikali ya Ujerumani pamoja na vyama vya upinzani kuwabana Wanazi mamboleo , kwa kupiga marufuku maandamano yao wakati wa maadhimisho ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji yaliyofanywa na Wanazi katika vita vikuu vya pili vya dunia, Holocaust.
Mabadiliko katika sheria ya haki ya kufanya mikutano itapelekwa katika bunge siku ya Ijumaa katika juhudi za kuwazuwia wanachama wa chama chenye msimamo mkali wa kulia cha NPD kuweza kuandamana katika lango la Brandenburg mjini Berlin hapo May 8.
Hayo yatakuwa maadhimisho ya mwaka 60 tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia katika bara la Ulaya.
Paul Spiegel, rais wa baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani amesema kuwa muswada wa sheria hiyo utaimarisha hadhi ya wahanga, utazilinda jamii ndogo ndogo hapa nchini , na kuilinda hadhi ya Ujerumani kimataifa isichafuliwe na wanazi mamboleo.