1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki ya Dunia yasitisha ufadhili wa utalii Tanzania

23 Aprili 2024

Benki ya Dunia imesitisha ufadhili wa mradi mkubwa wa utalii nchini Tanzania kwa madai kuwa umesababisha mateso miongoni mwa maelfu ya wanakijiji.

https://p.dw.com/p/4f5Lw
Benki kuu ya Dunia yasitisha ufadhili wa utalii Tanzania
Benki kuu ya Dunia yasitisha ufadhili wa utalii TanzaniaPicha: ullstein bild - Fotoagentur imo

Hii ni baada ya kundi moja la kutetea haki nchini Marekani kwa muda mrefu kumtaka mkopeshaji huyo wa kimataifa kuchukua hatua hiyo. 

Benki ya Dunia imechukua hatua ya kusitisha mradi huo wa dola milioni 150, ambao unalenga kuboresha usimamizi wa maliasili na utalii katika vijijini vya kusini mwa Tanzania.

Soma pia:Benki ya Dunia yashutumiwa kwa ukiukaji wa haki Tanzania

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Taasisi ya Oakland iliyokuwa ikiendesha kampeni hiyo imedai kwamba "kushindwa kuchukua hatua za haraka kulisababisha madhara makubwa kwa jamii."

Angalau dola milioni 100 zilikuwa tayari zimetolewa kwa mradi huo, ambao ulianza mwaka 2017 na hatua ya kusimamishwa kwake imeanza rasmi Aprili 18.

Shinikizo kutoka wanaharakati wa haki za binadamu na mazingira

Mbuyu katika Mbuga ya wanyama ya Ruaha, nchini Tanzania
Mbuyu katika Mbuga ya wanyama ya Ruaha, nchini TanzaniaPicha: picture-alliance/Lonely Planet

Taasisi ya Oakland, shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini California ambalo linaangazia jamii zilizotengwa, kwa miaka mingi imekuwa ikitoa wito kwa Benki ya Dunia kusitisha ufadhili wa mradi unaojulikanao kwa kifupi REGROW, kwa kwa madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki miongoni mwa wenyeji katika eneo hilo.

Kundi hilo katika ripoti iliyotolewa mwezi Novemba liliishutumu Benki ya Dunia kwa kushindwa kuziwajibisha mamlaka za Tanzania kwa kile ilichokiita "mauaji ya watu wengi na unyanyasaji wa kijinsia" wakati wa upanuzi wa Mbuga ya Wanyama ya Ruaha.

Ripoti hiyo ilisema mbinu za serikali ya Tanzania kulazimisha jamii kuondoka ili  kuongeza utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kama lengo la mradi wa REGROW, "zilisababishwa moja kwa moja na ufadhili wa Benki ya Dunia."

Benki ya Dunia ilisema wakati huo kwamba "haivumilii vurugu katika miradi inayoifadhili," na iliunda jopo la wakaguzi kupitia malalamiko yanayohusiana na mradi huo ili "kuamua kama maswala yaliyoibuliwa ni halali."

Ushindi kwa jamii zilizotengwa ?

Katika mawasiliano ya hivi majuzi kati ya Benki ya Dunia na Taasisi ya Oakland yaliyoonekana na shirika la habari la The Associated Press, mkopeshaji huyo alithibitisha kusimamishwa kwa malipo zaidi kwa mradi wa REGROW "hadi kuwe na uhakika kwamba mradi unazingatia viwango vya kijamii na kimazingira."

Anuradha Mittal, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Oakland, alisema uamuzi wa Benki ya Dunia kusitisha ufadhili ni ushindi kwa jamii zilizotengwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Mital ameongeza kuwa uamuzi huo unatuma ujumbe mzito kwa serikali ya Tanzania kwamba kuna matokeo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki unaofanyika kote nchini humo wakati ikiendeleza biashara ya utalii. Hata hivyo, mamlaka ya Tanzania haikutoa maoni kuhusiana na taarifa hii.