Benki ya Dunia: Ndoa za mapema zagharimu nchi nyingi mapato
6 Desemba 2018Jambo hili linazigharimu nchi mabilioni ya dola katika mapato yanayopotea. Makadirio ya nchi 12 yanaonyesha dola bilioni 63 zinapotea kwasababu wasichana wadogo walioolewa wanasoma kwa miaka michache ikilinganishwa na wenzao ambao wanaolewa baadae.
Ripoti hiyo iliopewa kichwa cha "Kuelimisha Wasichana na Kumaliza Ndoa za Utotoni" inasema kila mwaka wa elimu ya sekondari unapunguza kwa asilimia tano au zaidi uwezekano wa kuolewa kabla kutimu umri wa miaka 18.
Afrika Magharibi imetajwa kuwa na kiwango cha juu cha ndoa za kabla ya msichana kufikisha umri wa miaka 15 na fauka ya hayo, kati ya nchi ishirini zilizo na viwango vya juu vya ndoa za utotoni duniani, nchi 18 ni za Afrika.
Lengo la Umoja wa Afrika kumaliza ndoa za mapema halitatimia
Yvette Kathurima Muhia ni mkuu wa miadi Afrika katika shirika linaloitwa "Wasichana sio Mabibi" ambalo linajumuisha zaidi ya makundi 1,000 ya kijamii yanayoshughulikia suala hilo, anasema serikali zinastahili kushirikiana. Tangu Umoja wa Afrika kuanzisha kampeni ya kumaliza ndoa za utotoni kufikia mwaka 2023, nchi 24 zimezindua mikakati ya kitaifa kufikisha mwisho suala hilo.
Lakini Muhia anakiri kwamba lengo la Umoja wa Afrika la kumaliza ndoa za mapema kufikia mwaka 2023 haliwezi kutimia akisema juhudi kwa sasa zinakwenda polepole mno. Amesema mambo mengi zaidi yanahitajika kufanywa ili kuhakikisha wasichana wanasalia shule ikiwemo kuwapa mlo wa bila malipo, sodo na hata usafiri.
Ndoa za utotoni zinasababishwa na mambo mengi ikiwemo tamaduni, mabadiliko ya tabia nchi na mizozo, lakini umaskini ni sababu kubwa ambayo wengi hawaifahamu. Umoja wa Mataifa mwezi uliopita ulisema ukame magharibi mwa Afghanistan ambao umewaacha zaidi ya watu 250,000 bila makao, umeifanya hali mbaya ya kibinadamu kuwa mbaya zaidi, na kuzifanya baadhi ya familia kuwauzwa watoto wao wa kike ili walipe madeni au wanunue chakula.
Tamaduni katika jamii zinastahili kubadilika pia
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto UNICEF, karibu watoto 161 wa kati ya umri wa mwezi mmoja na miaka kumi na sita waliuzwa kati ya Julai na Oktoba.
Muhia anasema pamoja na kuangazia masuala ya sera na mabadiliko katika sheria tamaduni katika jamii ni sharti zibadilike pia.
Licha ya kampeni za uhamasisho zinazoendelea suala la kuwauzwa wasichana bado linaendelea na hivi majuzi msichana wa miaka 17 nchini Sudan Kusini aliwekwa mnadani katika mtandao wa kijamii wa Facebook jambo lililozua ghadhabu kote duniani. Tangazo hilo lilisambaa kwa haraka mitandaoni na hatimaye mtu aliyemzidi umri mara tatu ndiye aliyemuoa baada ya kutoa mahari ya kiasi kikubwa zaidi.
Miongoni mwa walioshiriki mnada huo katika mtandao wa Facebook alikuwa ni naibu gavana katika jimbo moja nchini humo.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga