Ofisi za kubadili pesa za kigeni kufungwa Burundi
11 Februari 2020Benki kuu ya Burundi imetowa muda wa hadi tarehe 15 mwezi huu wa Februari ofisi hizo za kubadili pesa za kigeni zifungwe kwenye maeneo yote ya umma.
Gavana wa benki hiyo Ciza Jean katika mkutano na waandishi wa habari, amezituhumu ofisi hizo za kubadilisha fedha za kigeni kwamba haziheshimu kanuni na Sheria zinazo agiza kuzingatiwa kiwango kilopangwa na Benki kuu ya Burundi katika ubadilishaji pesa ya kigeni.
Uamuzi huo wa benki kuu ya Taifa haujabaini hata hivyo njia mbadala ya kumuwezesha raia aidha mgeni mwenye pesa ya kigeni hata kiwango cha chini kujuwa wapi anaweza kubadilisha fedha hizo.
Swala la kudhibiti pesa ya kigeni inayoingia Burundi limekuwa tete mnamo miaka ya nyuma wakati serikali ikiamini kuwa pesa ya kigeni inachangia katika kuporomosha thamani ya faranga ya Burundi na kuvuruga uchumi.
Katika kipindi cha miezi 3 ya nyuma watu wa 3 wanao badili pesa za kigeni kinyume cha sheria waliuawa na watu ambao hadi sasa hawajajulikana.