1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yainyeshea Hamburg

Isaac Gamba
27 Februari 2017

Bayern Munich ilipata ushindi wa mabao 8-0 mwishoni mwa wiki  dhidi ya timu inayochechemea katika msimamo wa ligi ya kandanda ya Bundesliga Hamburg katika mchezo uliopigwa katika dimba la Allianz Arena mjini Munich

https://p.dw.com/p/2YJfi
Deutschland Bayern München vs Hamburger SV
Picha: Getty Images/Bongarts/L. Baron

Kiungo wa Bayern  Arturo Vidal ndiye aliyeanza kufungua karamu ya magoli na kufuatiwa na mabao mengine mawili yaliyofungwa na mshambuliaji machachari  mpolandi Robert Lewandowsk kabla ya dakika 45 za kwanza kumalizika. Robert Lewandowsk alipachika bao la nne muda mchache baada ya kuanza kipindi cha pili na kabla ya kupumzishwa alishirikiana vema na Thomas Muller kutengeneza bao la tano lililofungwa na David Alaba. Hata hivyo maumivu ya Hamburg hayakuishia hapo baada ya Robert Lewandowsk kupumzishwa kwani mshambuliaji mfaransa  Kingsley Coman alieingia  akitokea benchi alitikisa mara mbili nyavu za Hamburg kabla ya Mholanzi Arjen Robben kushindilia bao la nane na la mwisho lililoizamisha kabisa Hamburg katika pambano hilo.

Ushindi huo mnono wa Bayern umekuja baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na Hertha Berlin wiki iliyopita na sasa Bayern Munich wanaendelea kuongoza katika msiamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu ya RB Leipzig ambayo nayo iliishushia kisago cha mabao 3-1 FC Cologne katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Red Bull Arena.

Deutschland Valerien Ismael
Wolfsburg ilimtimua kocha Valerien IsmaelPicha: picture alliance/dpa/T. Eisenhuth

Borussia Dortmund nayo pia ilizidi kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza michuano ijayo ya kilabu bingwa barani ulaya pale ilipopata ushindi wa ugenini kwa kuikandamiza  Freiburg mabao 3-0. Bao la kwanza la Dortmund likifungwa na mgiriki Socrates aliyeunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na mshambuliaji Marco Reus kabla ya mgaboni Pierre- Emerick Aubameyang kupachika mabao mengine mawili na kuiwezesha timu hiyo kubeba pointi zote tatu muhimu katika pambano hilo.

Kocha Thomas Tuchel wa Dortmund alimsifia Aubameyang kwa kurejea tena katika form baada ya mshambuliaji huyo kuwa katika ukame wa mabao katika siku za hivi karibuni.

Hertha Berlin nayo iliwaba Eintracht Frankfurt mabao 2-0 huku Darmstadt inayo buruza mkia kwenye ligi hiyo ikizidi kujichimbia kaburi baada ya kuwaruhusu wageni Ausburg kuwachapa nyumbani mabao 2-1.

Schalke walikwenda sare ya 1-1 na Hoffenheim huku Gladbah wakiikwanyua Ingolstadt abao 2-0 nayo Werder Bremen ikaibanjua Wolfsburg mabao 2-1 katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyopigwa ijumaa.

Mwandishi: Isaac Gamba
Mhariri: Yusuf Saumu