1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern wachechemea katika Bundesliga

10 Januari 2022

Bayern Munich walipoteza mechi yao ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, walipochuana na Borussia Mönchengladbach mwishoni mwa wiki na kupelekea mwanya kati yao na Borussia Dortmund kupungua na kufikia pointi sita tu.

https://p.dw.com/p/45Ln8
Deutschland München | Bundesliga | Tor Florian Neuhaus
Picha: Imago Images/MIS

Hii ni baada ya Dortmund kupata ushindi wa 3-2 walipokuwa wakichuana na Eintracht Frankfurt ugenini. Bayer Leverkusen walikuwa nyumbani ila walilazimishwa sare ya magoli mawili walipokuwa wakikwaana na Union Berlin ambayo imempoteza mshambuliaji wao mahiri raia wa Nigeria Taiwo Awoniyi ambaye ameelekea kujiunga na timu yake ya taifa ya Nigeria kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa Barani Afrika huko Cameroon.

Hapo Jumapili FC Cologne waliwaadhibu Hertha Berlin magoli matatu kwa moja huko mjini Berlin Anthony Modeste akifunga goli la kwanza na lake la kumi na mbili la Bundesliga msimu huu. VfL Bochum walikuwa nyumbani na wakawazidi kete Wolfsburg 1-0 na kuwasogeza nafasi moja nyuma ya timu kumi bora kwenye msimamo wa Bundesliga.

Kwa sasa Bayern ndio walio uongozini wakiwa na pointi 43 Borussia Dortmund ni wa pili pointi zao zikiwa 37 halafu TSG Hoffenheim wamekwea hadi katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 31. Chini ya jedwali Augsburg, Arminia Bielefeld na Greuther Fürth ndio wanaovuta mkia.