Bayern Munich yatinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
18 Aprili 2024Bao la kichwa la Joshua Kimmich katika dakika ya 63 lilitosha kuwapa ushindi wa 1-0 Bayern Munich dhidi ya Arsenal na kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa katika mechi ya marudiano ya robo fainali iliyochezwa huko mjini Munich usiku wa kuamkia leo.
Kwa ujumla Bayern wametinga hatua hiyo ya nne bora kwa ushindi wa mabao matatu kwa mawili, baada ya mechi ya mkumbo wa kwanza baina ya timu hizo mbili kuishia sare ya magoli mawili kwa mawili katika uwanja wa Emirates huko mjini London.
Hii ndiyo mara ya kwanza Bayern kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo tangu walipolishinda taji hilo mwaka 2020 walipowafunga PSG katika fainali.
Soma pia:Dortmund na PSG zatinga nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya
Mshambuliaji wa Bayern Harry Kane ameutaja ushindi huo kuwa ni wa ajabu na kukiri kwamba ulikuwa ni msimu mgumu kwao kutokana na ukweli kwamba kuna nyakati fulani walilazimika kutofautiana, kwenye matokeo ya kuleta mabadiliko na kuwapa tabasamu mashabiki wao.
Akirejea katika bao la Kimmich amesema ni bao la kiufundi ambalo limewapa tiketi ya kutinga nusu fainali.
Bayern sasa itamenyana na Real Madrid katika nusu fainali.
Arsenal na kibarua kizito dimbani
Arsenal wamekuwa na matokeo ya kutoridhisha katika siku chache zilizopita baada ya kufungwa nyumbani na Aston Villa katika ligi kuu ya England mnamo siku ya Jumapili.
Matokeo hayo yaliwapelekea kupoteza uongozi wa ligi ya nchini humo na sasa wanashikilia nafasi ya pili katika jedwali linaloongozwa na Manchester City.
Sasa Bayern wametia pilipili kwenye kidonda chao. Tofauti na mchezo uliopita wa mabao manne mjini London, mechi ya jana Jumatano ilikuwa ngumu, huku kukiwa na nafasi chache za wazi kwa kila upande.
Kocha wa Arsenal Mikel Arteta alilazimika kufanya mabadiliko katika safu ya beki wa shoto akiamua kumtumia Mjapani Takehiro Tomiyasu badala ya Jakub Kiwior ili aweze kumdhibiti winga mwenye kasi wa Bayern, Leroy Sane.
Lakini Mjapani huyo alionekana kutofanya vyema na hatimaye kuondolewa uwanjani kunako kipindi cha pili.
Soma pia:Champions League yarudi tena, nani atatinga robo fainali?
Bayern Munich kwa upande wao walimkosa beki wao wa shoto Alphonso Davies ambaye kadi ya njano aliyoipata katika mechi ya kwanza huko London, ilimpelekea kupigwa marufuku kushiriki mechi ya jana. Nafasi yake ilichukuliwa na Raphael Guerreiro, aliyeishia kuwa mwandaaji wa goli la pekee la Bayern.
Ujerumani yajipiga kifua mbele baada ya matokeo
Kufuzu kwa Bayern kunaifanya Ujerumani kujivunia timu mbili katika hatua ya nusu fainali baada ya Borussia Dortmund Jumanne, kuwalaza Atletico Madrid na kufuzu kwenye hatua hiyo, ambapo sasa watacheza na PSG.
Katika robo fainali ya piliusiku wa kuamkia leo, Real Madrid ililipiza kisasi kwa Manchester City kwa kuifunga mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kustahimili vurugu kwenye Uwanja wa Etihad, mjini Manchester.
Mechi hiyo iliishia sare ya bao moja kwa moja katika muda wa kawaida na wa ziada, baada ya nyota wa Brazil Rodrygo kuiweka Madrid kifua mbele kunako kipindi cha kwnaza cha mechi.
City ambao waliumiliki mpira pakubwa katika mechi hiyo, walisawazisha kupitia kiungo wao mahiri Kevin De Bruyne kunako dakika ya 76.
Hatua ya mikwaju ya penalti ilishuhudia Real Madrid kukosa mkwaju wao wa kwanza kabisa uliopigwa na mkongwe Luka Modric. Lakini City nao waliishia kukosa mikwaju miwili iliyopigwa na Bernardo Silva na Mateo Kovacic.
Madrid walifunga penalti zao zote zilizosalia huku Antonio Rudiger akifunga mkwaju wa mwisho na kuwapelekea vinara hao wa ligi kuu ya Uhispania, kulipiza kisasi cha kutolewa na City msimu uliopita, na kutinga nusu fainali.
Soma pia:Man U yatupwa nje michuano ya Champions League
Kuondolewa huku kwa City kunawanyima fursa ya kulitetea taji waliloshinda msimu uliopita ambao ulikuwa wa kihistoria kwao, kwani walishinda mataji matatu.
Real Madrid ndiyo timu ya pekee katika historia kulitetea taji hilo la ligi ya vilabu bingwa.
Mechi za nusu fainali sasa zitachezwa Jumanne na Jumatano ya tarehe 30 Aprili na Mei mosi na fainali ya mashindano hayo itachezwa nchini England katika uwanja wa Wembley.